MTAZAMO WA VIONGOZI WA AFRIKA KWA BABA WA TAIFA, MWALIMU NYERERE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 14 October 2019

MTAZAMO WA VIONGOZI WA AFRIKA KWA BABA WA TAIFA, MWALIMU NYERERE

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere.

Huu ndio mtazamo wa viongozi wa Afrika kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere 

RAIS wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe,  kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa Afrika, alikuwa na mapenzi makubwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere kutokana na kuzisaidia nchi za kusini mwa Afrika kupata uhuru.

Kutokana na kuthamini kwake mchango huo wa Mwalimu Nyerere, yeye na viongozi wengine kadhaa wa Afrika, walipendekeza moja ya majengo ya Umoja wa Afrika (AU), yaliyoko Addis Ababa, Ethiopia, kupewa jina lake.

Mwalimu Nyerere alipewa heshima hiyo kutokana na mchango wake katika ukombozi na kuliondoa Bara la Afrika katika ukoloni.

Uamuzi wa kuliita Jengo la Baraza la Amani na Usalama laumoja huo jina la Mwalimu Julius Nyerere Hall, ulifikiwa wakati wa kikao cha ndani cha marais wa nchi wanachama wa AU, kilichofanyika Ethiopia.

Hoja ya kuliita jengo hilo Mwalimu Nyerere, iliwasilishwa na Rais wa Namibia, Hifekepunye Phohamba, katika kikao cha Baraza la Amani na Usalama na kufafanuliwa na Rais Mugabe.

Akizungumza katika kikao hicho kwa lugha ya kuvutia ya Kiingereza na mifano mingi ya kuchekesha, Rais Mugabe alisema: “Naweza kuandika kitabu hata hapa hapa kuhusu mchango wa Mwalimu na Tanzania katika ukombozi wa Bara letu, hasa Kusini mwa Afrika.”

“Nchi gani ingeweza kubeba mzigo mkubwa kiasi hiki? Idadi ya vyama vya ukombozi na vijana wake na vurugu zao za kawaida, idadi ya wakimbizi kutoka nchi mbalimbali na wala siyo nchi tajiri. Kamwe hatutasahau mchango huu mkubwa waliotufanyia,” alisema.

Kuna wakati Mugabe aliwahi kupingana hadharani na wanadiplomasia wa nchi za magharibi wanaomtambua Nelson Mandela kama mkombozi wa Afrika.

Mugabe aliwaeleza wazi kuwa, mkombozi halisi wa Afrika ni Mwalimu Nyerere kwa sababu hata Mandela alisaidiwa na Nyerere kupata ukombozi wa nchi yake.

Alisema Mandela alipigania ukombozi wa Afrika Kusini pekee,wakati Nyerere alijikita kuzisaidia nchi zingine za kusini mwa Afrika zipate uhuru wake.

Mugabe aliongeza kuwa, wanajeshi kutoka Msumbiji, Zambia, Malawi, Angola, Zimbabwe, Namibia, Botswana na Afrika Kusini, waliishi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ikiwemo Dakawa, Kongwa, Mtwara, Songea, Mbeya na Dar es Salaam huku wakipewa msaada na mafunzo ya kijeshi.

No comments:

Post a Comment