KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sekta ya Ujenzi kwa kupeleka fedha za kutosha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ili kuuwezesha Wakala huo kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, mjini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza Wakala kujipanga na kutekeleza kwa vitendo mipango waliyoianzisha badala ya kuishia kwenye makaratasi.
"Kamati imepaza sauti na fedha za kutosha mmeshapewa sasa mfanye kazi kwani hatuhitaji mipango mizuri ya makaratasi bali tunataka vitendo", amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Aidha, ameitaka Wizara ishirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inasimamia madai ya kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 31 ambayo Wakala huo unadai Taasisi za Serikali na Wizara ili yalipwe kwa wakati.
Mwenyekiti ameongeza kuwa Wizara itizame katika mapana yake namna bora ya kupunguza gharama za ununuzi wa magari pamoja na vipuri vyake kwa kuwa lengo ni kuipunguzia gharama Serikali.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amewaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa TEMESA ilifanikiwa kukusanya mapato ya kiasi cha zaidi ya shilingi Bili 58 kutoka vyanzo vyake vya ndani vya mapato na ruzuku ya Serikali.
Ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha 2019/20 Wakala unatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 89. Naibu Waziri huyo amesema Wakala umeanzisha karakana katika ngazi ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ili kuhakikisha huduma inasogezwa karibu na wateja.
Ameongeza kuwa Wakala umenunua vitendea kazi vya kisasa ikiwemo gari lenye karakana (Mobile Workshop) ambalo litatoa huduma popote pale na pia Wakala ulikamalisha ukarabati wa karakana za Mkoa wa Singida, Dar es Salaam na Mwanza.
Naye Mbunge wa Misungwi, Mheshimiwa Charles Kitwanga, amesisitiza umuhimu wa usalama wa abiria na mizigo katika vivuko kwa kuweka na mifumo madhubuti ya kuonesha idadi kamili ya abiria na uzito wa mizigo ili kuepusha ajali zinazoweza epukika.
Kikao cha Kamati hiyo kimeshirikisha wajumbe mbalimbali ikiwemo Naibu Waziri wa Sekta ya Ujenzi Elias Kwandikwa, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga ambapo taarifa ya utekelezaji ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ambayo inatokana na maazimio ya vikao vya Bunge vilivyopita imejadiliwa na kupokelewa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment