WAZIRI MKUU AAGIZA GARI LA WAGONJWA LIPELEKWE IFAKARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 17 September 2019

WAZIRI MKUU AAGIZA GARI LA WAGONJWA LIPELEKWE IFAKARA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na ni mke wake, Mary Majaliwa (kushoto), akizungumza na wananchi, wakati alipokagua kituo cha Afya Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Septemba 17.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Septemba 17.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka gari la kubebea wangonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kukodi gari kwa sh. 800,000 pale wagonjwa wao wanapopata rufaa.

Wananchi wa Mji wa Ifakara wameiomba  Serikali iwasaidie kuwapatia gari la wagonjwa kwani kitua chao hakina gari na wagonjwa wao wanapopata rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro wanalazimika kukodi gari kutoka hospitali ya Mtakatifu Francis kwa gharama ya sh. 800,000 ambazo baadhi yao wanashindwa kuzimudi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kituo cha mabasi cha mji huo. Amesema iwapo fedha za makusanyo ya mapato ya ndani  katika halmashauri husika zingekuwa zinatumika vizuri kusingekuwa na changamoto  kama hizo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao kuendelea kuwa na imani na Serikali yao. “Nitampigia simu Waziri Ummy (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) katika mgao ujao alete gari la wagonjwa hapa.”

Pia, Waziri Mkuu ameielekeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe katika mgawo wa ujenzi wa hospitali za wilaya, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipewe kipaumbele kwa sababu eneo hilo ni kubwa na lina watu wengi lakini hakuna hospitali ya wilaya hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

“Nimetembelea mwenyewe kituo cha Afya cha Kibaoni na nimeshuhudia msongamano wa wagonjwa, mgao wa pili wa ujenzi wa hospitali za wilaya Mji wa Ifakara lazima upewe kipaumbele. Suala la huduma za afya ni suala nyeti, hivyo ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”

Awali, Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Happyness Ndosi alisema kituo cha Afya cha Kibaoni kinapokea na kuwahudumia wagonjwa wa  nje 225 hadi 250 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku. Wakinamama wanaojifungulia kituoni hapo ni 400 kwa mwezi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazikabili kituo hicho amesema kina upungufu wa watumishi 92, kwani kina jumla ya watumishi 83 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 175,  ukosefu wa gari la wagonjwa na pia hakina gari lolote la kutolea huduma zikiwemo za chanjo, na usambazaji, uchakavu kwa baadhi ya majengo kama la wagonjwa wa n je.

Pia, kituo kinakabiliwa na ukosefu wa jengo la kutunzia watoto njiti, watoto wachanga na wale wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kuzaliwa (neonatal unit), ufinyu wa chumba cha kujifungulia pamoja na ukosefu wa mashine ya kutolea dawa za usingizi (anesthesia machine).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali haitokuwa na msamaha  na watendaji wa halmashauri watakaobainika kutafuna fedha za makusanyo ya mapato ya ndani pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.

“Fedha za mapato ya ndani hazitumiki vizuri watu wanadukua mifumo, wanapaswa watambue kwamba Serikali ipo makini wakati wote. Watumishi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo vya ubadhilifu hatua kali za kinidhami zitachukuliwa dhidi yao. Watumishi wa umma mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi.”

Waziri Mkuu amesema watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha na  migogoro kwa kuwa ni kunyume na taratibu za kiutumishi. “Haiwezekani viongozi wakagombania zabuni zitokanazo na fedha za kodi za wananchi, kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Serikali itasimamia zabuni zote.”


 WAKATI HUO HUO; Kassimu Majaliwa amesema hajaridhishwa na gawio la sh milioni 800 linatolewa na kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho uzalishaji wake ni kikubwa ikilinganishwa na kiwanda cha sukari cha Moshi TPC ambacho kinatoa gawio la sh. billion 15 kwa mwaka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho, akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro. Amevitaka viwanda vya sukari nchini kuzaliza sukari ya kutosha ili kukidhi mahitaji.

Akizungumzia kuhusu vibali vya uagizaji wa sukari, Waziri Mkuu amesema Serikali iliamua kutoa nafasi ya kuagiza sukari kwa wenye viwanda ili kuepuka ujanja uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa wakiagiza sukari kutoka nje ya nchi ambayo nyingine ilikuwa haina ubora.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania bado kuna uhitaji mkubwa wa sukari hususani ya viwandani, hivyo kusababisha Serikali kutoa vibali kwa wamiliki wa viwanda kuagiza sukari kutoka nje ya nchi. “Viwanda vya ndani vya sukari vihakikishe vinaongeza uzalishaji wa sukari ya viwandani ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema mahitaji ya sukari kwa mwaka huu nchini yameongezeka hadi kufikia tani 710,000 ikilinganishwa na tani 610,000 za mwaka jana.

Amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa viwanda vipya vinavyotumia sukari ya viwandani, ambapo kwa sasa mahitaji ya sukari ya viwandani yamefikia tani 165,000. 

Amesema mahitaji ya sukari za majumbani kwa sasa ni tani 545,000, ambapo kiwanda cha Kilombero kinazalisha tani 134,000, kiwanda cha Manyara tani 6,000, kiwanda cha Mtibwa tani 39,000 na TPC cha Moshi tani 100,000.

Naibu Waziri huyo amesema ili kukabiliana na upungufu wa sukari Serikali imeweka mkakati wa kuanzishwa kwa viwanda vipya vya sukari vya Bagamoro ambacho kitaanza kuingiza awamu ya kwanza ya sukari sokoni tani 35,000 ifikapo mwaka 2022 na kiwanda cha Mkulazi kinatarajiwa kuzalisha tani 200,000 na cha Mbigili tani 50,000.

Akitoa taarifa za kiwanda hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari Balozi Amry amesema Kampuni ya Sukari ya Kilombero imezingatia kikamilifu wito wa Serikali wa kukuza uzalishaji na kuweka mipango thabiti ya upanuzi wa uzalishaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha kusindika miwa. Mradi huo utagharimu sh. bilioni 700.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu ametoa muda wa wiki mbili kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa awe amechimba visima katika kata ya Ruaha kwa ajili ya kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kupata maji safi na salama.

Ameyasema hayo baada ya wakazi wa kata hiyo kusimamisha msafara alipokuwa akielekea kata ya Malolo. Amesema halmashauri hiyo inakusanya zaidi ya sh. bilioni mbili kwa mwaka hivyo inatakiwa kutenga kiasi cha fedha za mapato kugharamia miradi ya maendeleo ya wananchi.

Waziri Mkuu amesemaSerikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambayo inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na maeneo yao.

No comments:

Post a Comment