MBUNGE wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba leo tarehe 17 Septemba 2019 amewataka wananchi kushirikiana katika ujenzi wa maendeleo wa wilaya hiyo na kutumia vizuri vifaa vya ujenzi anavyozidi kuvitoa katika wilaya hiyo ili kuwezesha maendeleo kukua na kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili, ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi vifaa vya ujenzi wakati wa ziara katika jimbo hilo.
Mwigulu alisema kuwa upo umuhimu wa kutunza vifaa hivyo na kuvitumia vizuri katika shughuli zilizo elekezwa kwani kuna baadhi ya watu wasio penda maendeleo wanaotumia misaada inayotolewa kwaajili ya shughuli za maendeleo katika shughuli zao binafsi.
Aidha, aliongeza kuwa jimbo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto ya baadhi ya shule kukosa mabweni na ukilinganisha kuwa zipo mbali hivyo kuwa kadhia kubwa kwa wanafunzi jambo lililomfanya kuwa na mkakati ikiwemo kutoa fedha na baadhi ya vifaa ili kuhakikisha angalau kila shule inakuwa na mabweni kwa ajili ya kusaidia watoto wa kike wanaotoka umbali mrefu na baadae kujengwa mabweni ya watoto wa kiume.
Alisema kuwa kwa wanafunzi kusomea majumbani ni changamoto kwao kwani wanakosa muda kwaajili ya kujisomea na kujikuta wakiishia kufanya shughuli za nyumbani ukiachilia mbali watoto wakike kupata ujauzito kwa kubakwa au kudanganywa wakiwa njiani.
“Ninajitoa kuhakikisha naboresha huduma za elimu kila kata na kila shule ili wanafunzi wetu ufaulu uongezeke sasa natoa onyo ole wake kijana atakaemsumbua mtoto wa kike au kumpa ujauzito miaka 30 itakuhusu na sina mchezo kwenye hili’’ Alisema Mwigulu.
Pia alibainisha kuwa amejipanga kuhakikisha anachangia na kuhamasisha wananchi ili kuhakikisha anaboresha sekondari za kidato cha sita katika wilaya hiyo kwa kushirikiana na wananchi hivyo amewaomba kutoa ushirikiano.
Kadhalika, katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana katika kila kijiji na kata alisema kuwa katika ziara hiyo atatoa baadhi ya vifaa ili kusaidia kukamilisha zahanati ya Shelui ikiwemo saruji mifuko miamoja na fedha taslimu milioni moja na nusu pia ameahidi kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuwasaidia wananchi kuondoa adha ya kukosa huduma za afya.
Awali, wakati wa kuanza ziara yake mapema alishiriki katika makabidhiano ya msaada wa mabati 175 katika shule ya sekondari Kinambeu kwa ajili ya kumalizia jengo la hosteli lililo ungua kwa moto Septemba 2018 kutoka kwa NMB ambapo aliwashukuru kwa kuzidi kuisaidia jamii na kumuunga mkono katika kuleta maendeleo kwenye jamii.
Mbunge huyo wa Jimbo la Iramba Magharibi Mhe Mwigulu Nchemba ameendelea na ziara ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake huku ikishuhudiwa makundi ya mamia wakimlaki na kushiriki katika mikutano ya hadhara anayoifanya katika kila kijiji, ziara hizo zinatarajiwa kuendelea tena kwa siku mbili mfululizo.
No comments:
Post a Comment