Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (MB) akitembelea maonesho anuai ya shughuli za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye uzinduzi huo. |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (MB) akitembelea maonesho anuai ya shughuli za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye uzinduzi huo. |
Na Joachim Mushi
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (MB) leo ameizinduwa rasmi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania “Tanzania Meteorological Authority (TMA)” ambapo awali mamlaka hiyo ilikuwa ikifanya kazi kama wakala wa hali ya hewa nchini "Tanzania Meteorological Agency".
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Ubungo Plaza na kuambatana na uzinduzi rasmi wa mifumo mitatu, yaani “TMA Digital Meteorological Observatory (TMA-DMO)” kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano ya Data za Hali ya Hewa; “Meteorological Aviation Information System (MAIS)” kwaajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za hali ya hewa katika usafiri wa anga na “Marine Meteorological Information System (MMIS)”, mfumo unaosaidia katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya majini yaani bahari, maziwa na mito.
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Kamwelwe alisema taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana kwa ajili ya shughuli za kiuchumi zikiwemo za kilimo, uvuvi, usafiri hususani wa anga na majini, pia shughuli nyingine za kijamii kama kutoa tahadhari ya majanga.
"Serikali itaendelea kushirikiana na kuiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Katika kuboresha huduma zake Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania, "Tanzania Meteorological Agency" sasa imepandishwa hadhi na kuwa Mamlaka. Lengo likiwa ni kuiwezesha mamlaka kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuwa na wigo mpana zaidi wa kuzingatia maslahi ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani...," alisema Waziri Kamwelwe.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dk. Agnes Lawrence Kijazi alisema Uzinduzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni ishara ya mwendelezo wa kazi nzuri na huduma zinazotolewa na TMA.
Aidha Mamlaka imeongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu utoaji na utumiaji wa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alibainisha kuwa Wakala wa Hali ya Hewa ambao unafikia ukomo wake rasmi leo ulianzishwa mwaka 1999 kwa Mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali sura 245 marejeo ya 2002.
Ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini Serikali imeona ni vyema kuhuisha shughuli za Wakala na kuwa Mamlaka kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora zaidi za hali ya hewa nchini na pia kukidhi mahitaji ya sasa ya utoaji na matumizi ya hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"...Katika kipindi cha Wakala, tumepata mafanikio makubwa ambayo yanahitaji kuendelezwa tunapoingia katika Mamlaka. Mafanikio haya ni pamoja na kupata vyeti vya ubora vya utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa viwango vya kimataifa katika sekta ya usafiri wa anga yaani ISO 9001:2008 ambacho kilipatikana mwaka 2011 na;
Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa Taasisi za hali ya hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho, na ISO 9001:2015 ambacho kilipatikana mwaka 2017 na Tanzania ilikuwa nchi ya tatu Afrika kupata cheti hicho, kusimikwa kwa Radar mbili za hali ya hewa na Rada nyingine tatu zikiwa katika hatua ya ununuzi. Alisema Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
No comments:
Post a Comment