Mtaalamu wa Hali ya Hewa, Bi. Veronica Mgalula (kushoto) akifanya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa kwa wanahabari kabli ya kutolewa utabiri huo. |
Sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TMA, wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na wanahabari wakiwa katika mkutano huo leo jijini Dar es Salaam. |
Na Joachim Mushi
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo jijini Dar es Salaam imetoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli, kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba, 2019.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes L. Kijazi amesema mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwasasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2019 - mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na Pwani ya kaskazini.
Amesema ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (Kibondo) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini yakitarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Amebainisha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. Kanda ya Ziwa Viktoria mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga.
"...Maeneo machache ya mkoa wa Kagera mvua za nje ya simu zinaendelea toka mwezi Agosti na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine ya ziwa Viktoria hadi kufikia wiki ya pili ya mwezi Oktoba, Hivyo kuungana na msimu wa mvua za Vuli.
Mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba. Kiwango cha mvua kinachotarajiwa katika msimu huu ni mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda huo," alisema Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Kijazi.
Aidha alibainisha kuwa msimu wa mvua za vuli katika maeneo haya unatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2020. Alisema kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro; mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu.
Vipindi virefu vya ukavu na mvua chache pia vinatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini. Hata hivyo, mvua zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha wastani kuanzia wiki ya pili ya mwezi Novemba. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba.
Kwa upande wa Nyanda za juu Kaskazini Mashariki katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba 2019.
Kwa upande wa tahadhari, TMA imesema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevu nyevu ardhini unatarajiwa kujitokeza pamoja na upungufu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo hivyo kuna uwezekano wa kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Pamoja na hayo, aliongeza kuwa wafugaji wanashauriwa kuvuna mifugo yao ikiwa bado katika hali nzuri. Wafugaji pia wanashauriwa kutunza mifugo yao kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa ugani katika maeneo yao.
"...Sekta ya uvuvi, katika maeneo hayo, inaweza kuathiriwa kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya samaki na hivyo wafugaji wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya ufugaji wa samaki na kuzingatia matumizi sahihi ya maji.
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, shughuli za kawaida za kilimo zinatarajiwa. Aidha, malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa."
No comments:
Post a Comment