SERIKALI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA DARAJA LA MAGARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 3 September 2019

SERIKALI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA DARAJA LA MAGARA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S China Railyway Seventh Group anayejenga Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami, wakati alipotembelea na kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Mkoani Manyara. 

Meneja wa Wakala wa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara Eng. Bashiri Rwesingisa, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, wakati alipotembelea na kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami, Mkoani Manyara.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4.

Katibu Mkuu Mwakalinga, amesema kuwa daraja hilo linajengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group kwa muda wa miezi ishirini na sita (26)  na kuongeza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwani litaunganisha Wilaya ya Mbulu na Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara.

Amefafanua pia daraja hilo litaunganisha hifadhi ya Taifa ya Manyara na Tarangire kupitia Mayoka pamoja na kuunganisha mashamba makubwa ya mpunga na miwa yaliyopo ng'ambo ya pili ya Mto na masoko ya Babati, Arusha na kwingineko kwa vipindi vyote vya mwaka.

Katibu Mkuu ameyazungumza hayo katika eneo la Magara, mkoani Manyara ambapo pamoja na mambo mengine alipokea taarifa ya mradi kutoka kwa Mshauri Elekezi M/S Crown Tech Consult na kukagua hatua za ujenzi wa daraja hilo na kusisitiza kwa mkandarasi kukamilisha daraja hilo kwa mujibu wa mkataba.

"Nimeridhishwa na kazi zilizofanyika mpaka sasa, naomba Meneja wa TANROADS endelea kusimamia daraja hili likamilike kwa muda uliopangwa", amesisitiza Arch. Mwakalinga.

Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo la Magara utachochea ukuaji wa utalii na uchumi  katika mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla.

Arch. Mwakalinga, ametoa wito kwa wananchi wa Magara kuendelea kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ikiwa ni pamoja na kutojihusisha na vitendo vya wizi wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa Daraja.

"Nitoe wito kwa wananchi wa maeneo haya kuwa daraja pamoja na miundombinu yake ni mali ya umma hivyo ni jukumu la wananchi kuilinda na kuitunza", amesema Arch. Mwakalinga.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara Eng. Bashiri Rwesingisa, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa ujenzi wa daraja hilo unatarajia kukamilika mwezi Februari mwakani na unagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 12.

Eng. Rwesingisa ameendelea kueleza kuwa hatua za mradi mpaka sasa zimefikia asilimia 75 na kazi nyingi zimefanyika ikiwemo kuweka mihimili ya chuma kwa ajili ya kubeba zege la juu la Daraja limekamilika asilimia 100.

Ameongeza kuwa katika mradi huo mkandarasi atatakiwa kuhakikisha mazingira ya Mto Magara yanakuwa salama hii ikiwa ni pamoja na kupanda miti ili kuufanya mto huo usihame.

Daraja la Magara lipo umbali wa KM 21 kutoka Mbuyu wa Mjerumani katika barabara kuu ya Babati - Arusha ili kuwezesha kuvuka mto Magara katika barabara ya Mkoa ya Mbuyu wa Mjerumani - Mbulu yenye urefu wa KM 49.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment