SERIKALI INATAMBUA UMUHIMU WA LUGHA ZA ALAMA-MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 28 September 2019

SERIKALI INATAMBUA UMUHIMU WA LUGHA ZA ALAMA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua   Urasimishaji wa Lugha za Alama Tanzania katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani kwenye uwanja wa Kichangani, Kihesa mjini Iringa, Septemba  28, 2018. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happy. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama ili kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo itaendelea kusimamia uendelezaji, usanifu na urasimishaji wa Lugha ya Alama ya Tanzania, ambao ameuzindua Septemba 28, 2019

Amesema hatua hiyo itawezesha utoaji wa elimu katika ngazi mbalimbali pamoja na kuboresha mawasiliano katika jamii na tayari imetoa mafunzo ya lugha hiyo awamu ya kwanza kwa walimu 82 wa shule za Sekondari nchini na kwamba zoezi hilo ni endelevu.

Ameyasema hayo Septemba 28, 2019 wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani katika Uwanja wa Kichangani – Kihesa, wilayani Iringaakiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. 
Kaulimbiu ya siku ya Viziwi Duniani kwa mwaka huu inasema “Haki ya Matumizi ya Lugha ya Alama kwa wote”. Kaulimbiu hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya mawasiliano miongoni mwa Watanzania ambao ni Viziwi.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kurasimisha Lugha ya Tanzania, kutayarisha vifaa vya kufundishia Lugha ya Alama ya Tanzania na kufundisha walimu katika shule za Msingi na Sekondari nchini. Mchakato huo utachukua muda wa takribani miaka miwili kukamilika.”

Amesema Serikali itahakikisha kuwa lugha ya alama ya Tanzania inatambulika na kutumika kikamilifu kama chombo cha mawasiliano miongoni mwa Viziwi nchini ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa lao. 

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria na inatekeleza kwa dhati jitihada za kutoa kipaumbele kwa Watanzania wanyonge ambao hawakuwa wakinufaika ipasavyo na rasilimali za nchi. 

“Serikali yenu sikivu inatambua vikwazo vya aina hiyo na inatekeleza maelekezo ya Ilani ya CCM ya 2015/2020, ambayo inaielekeza Serikali ihakikishe watu wenye ulemavu wanapata elimu kwa kupata vifaa maalumu na kushiriki katika shughuli za kijamii.”

Hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu na mazingira rafiki yatakayowawezesha watu wenye ulemavu kwenda wanapotaka, kutumia vyombo vya usafiri na kupata habari kama walivyo wengine. Amesema katika ofisi yake ataajiri mkalimani wa lugha za alama.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi kwa kutumia lugha ya alama, alama mguso, maandishi ya nukta nundu, maandishi yaliyokuzwa au njia nyingine zinazofaa.

Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kurasimisha Lugha ya Tanzania, kutayarisha vifaa vya kufundishia Lugha ya Alama ya Tanzania na kufundisha walimu katika shule za Msingi na Sekondari nchini. Mchakato huo utachukua  takribani miaka miwili kukamilika.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na shule maalumu ya Serikali ambayo inahudumia watoto wenye mahitaji maalumu imeanza ujenzi wa Shule Maalumu Patandi katika Mkoa wa Arusha. Shule hiyo inatarajiwa kuchukua wanafunzi 600 wa Msingi na Sekondari na itagharimu sh. bilioni 2.8.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika mapitio ya Kanuni za Maudhui ya Vyombo vya Habari, Kanuni za mwaka 2011, Serikali imeingiza kipengele kipya kinachovitaka vyombo vyote vya habari kuwa na wakalimani wa lugha ya alama kwa vipindi muhimu. Baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo Shirika la Habari Tanzania (TBC) vimekuwa vikitekeleza agizo hilo. 

“Napenda kutumia maadhimisho haya kuagiza vyombo vyote vya habari kuhakikisha kwamba agizo hili linatekelezwa ipasavyo. Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kuwa haki na mahitaji ya Watu wenye Ulemavu vinapatiwa ufumbuzi kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010.”

Amesema anajua ajua changamoto wanazokumbana nazo viziwi wanapotaka kupata huduma mbali mbali katika vituo vya kutolea huduma za afya, mahakama, vituo vya polisi, nyumba za ibada na maeneo mengine muhimu kwa kuwa hayana wakalimani wa lugha ya alama.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi zote za Serikali na binafsi zihakikishe zinakuwa na wakalimani wa lugha ya alama. “Pia naagiza kwamba mitaala ya vyuo vya Afya, Polisi, Mahakama na vinginevyo ihakikishe inazingatia kuongeza kozi ya Lugha ya Alama kama somo la lazima. Hii itasaidia kuzalisha watalaamu wa lugha ya alama ambao wataweza kuwahudumia wenzetu viziwi ipasavyo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Nidrosy Mlawa ameishukuru Serikali kwa kuwaamini watu wenye ulemavu na kuwateuwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi, lakini waomba iongeze nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu ili nao waweze kujikwamua kiuchumi na kusaidia Taifa.

Pia, ameiomba Serikali iwe na wakalimani wa lugha za alama kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu waweze kupata taarifa zinazolewa na viongozi wao. Wameomba Serikali ikamilishe mchakato wa urasimishaji wa Lugha ya Alama ya TanzaniaWaziriMkuu amesemamaombi na mapendekezo yao ni ya msingi na muhimu kwa maisha ya Viziwi. Lengo la Serikali ni kuboresha huduma zetu kwa Viziwi hapa nchini. 

Maadhimisho hayo yamehudhuliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Josephat Kandege, Naibu Waziri - Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye UlemavuStela Ikupa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu pamoja na viongozi wa CHAVITA.

No comments:

Post a Comment