WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AKAGUA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA WAZIRI MKUU KUHUSU UNUNUZI WA PAMBA KATIKA WILAYA YA BARIADI, ITILIMA NA MASWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 8 August 2019

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AKAGUA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA WAZIRI MKUU KUHUSU UNUNUZI WA PAMBA KATIKA WILAYA YA BARIADI, ITILIMA NA MASWA


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wananchi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu kukagua utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa hivi karibuni kwa wafanyabiashara kununua Pamba ya wakulima, tarehe 6 Agosti 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal)



Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wananchi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu kukagua utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa hivi karibuni kwa wafanyabiashara kununua Pamba ya wakulima, tarehe 6 Agosti 2019.


Na Mathias Canal, Simiyu

WAZIRI
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) tarehe 6 Agosti 2019 amefanya ziara ya kikazi mkoani Simiyu kukagua utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa hivi karibuni kwa wafanyabiashara kununua Pamba ya wakulima.

Mhe Hasunga ametembelea na kukagua Kituo cha ununuzi wa Pamba cha Itemelo kilichopo kata ya Dutwa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Kituo cha ununuzi cha Lugulu katika kata ya Lugulu Wilaya ya Itilima na Kituo cha Kumalija kilichopo katika kata ya Shanwa wilayani Maswa.

Katika ziara hiyo Mhe Waziri amejionea hali ya ununuzi wa Pamba ya wakulima ukiwa unaendelea kutokana na serikali hivi karibuni kupata muarobaini wa mustakabali wa zao hilo. Waziri huyo wa Kilimo amepiga marufuku Pamba ya wakulima kupimwa katika mizani zisizofahamika badala yake lazima ipimwe katika mizani iliyothibitishwa na wakala wa vipimo.

Katika hatua nyingine pia Mhe Hasunga ametoa kalipio Kali kwa wanunuzi wa Pamba kadhalika vyama vya ushirika vinavyowakata kilo moja wakulima kwa madai ya mifuko ya kupimia badala yake ameagiza mkulima akatwe kutokana na uzito wa mfuko sio kukadiria kilo moja.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kuwanufaisha wakulima kupitia mazao wanayozalisha kwa kuwaongezea elimu ya Kilimo bora na chenye tija.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga yupo mkoani Simiyu kwa ajili ya sherehe za wakulima (Nanenane) ambazo kilele chake ni tarehe 8 Agosti 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa kufunga maadhimisho hayo akimuwakilisha Rais wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.

No comments:

Post a Comment