*UCHELEWESHWAJI MALIPO YA WAKULIMA KUWA HISTORIA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza Agosti 8, 2019 kwenye maonyesho ya Nanenane katika kilele cha siku ya wakulima Uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Agost 8, 2019 amekagua ununuzi wa pamba katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Itemelo kwenye kijiji cha Dutwa mkoani Simiyu. |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanunuzi wa zao la pamba katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanaongeza kasi ya ununuzi wa zao hilo ili wakulima waweze kupata fedha zao kwa wakati.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na Manaibu Waziri wake kubaki katika mikoa yote inayolima zao la pamba hadi wakulima wote watakapolipwa fedha zao na kuhakikisha pamba yote iliyomo mikononi mwa wakulima inauzwa.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati alipotembelea Chama cha Msingi cha Itemelo kilichoko eneo la Dutwa wilayani Bariadi, Simiyu kwa ajili ya kujionea mauzo ya zao la pamba.
Waziri Mkuu amesema ataendelea kusimamia mwenendo wa zao hilo kwa ukaribu lengo likiwa kuona wakulima wananufaika kwa kupata tija. “Ilani ya CCM ya 2015/2020 inasisitiza kilimo na inataka wakulima wapate masoko ya uhakika na tunalitekeleza jambo hilo na pamba yote itanunuliwa.”
Amesema Serikali inataka kuona pamba yote iliyoko kwa wakulima inatoka ili wakulima waweze kulipwa fedha ambazo zitawawezesha kujikimu kimaisha pamoja na kununua pembejeo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa AMCOS wahakikishe wanawatambua wakulima kwa majina, maeneo wanayoishi pamoja na ukubwa wa mashamba yao ili waweze kuagiza pembejeo kulingana na mahitaji halisi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kufungua akaunti katika taasisi mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kuhifadhi vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya pamba ili ziweze kuwasaidia baadaye.
Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wakulima hao waendelee kutunza vizuri pamba yao na kuipeleka ghalani ikiwa katika hali nzuri ya usafi na ubora wa hali ya juu, kwani kwa sasa pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora katika soko la dunia.
Kwa upande wa masoko hususan ya pamba, Waziri Mkuu aliwasisitizia wananchi wa Dutwa na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli inaendelea kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika wa mazao yote hususan yale ya kimkakati.
Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa moja ya agenda muhimu ya ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Misri mwezi Julai 2019 ilikuwa ni kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya Tanzania likiwemo na zao la pamba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally alipokaribishwa kuwasalimu wananchi alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa msukumo katika ununuzi zao la pamba. Aidha alimuomba Waziri Mkuu aongeze msukumo zaidi ili wakulima walipwe fedha zao kwa wakati.
Naye,Waziri wa Kilimo Hasunga amesema kuwa hali ya malipo kwa wakulima wa zao la pamba kwa sasa ni ya kuridhisha kwa kuwa wakulima katika maeneo mbalimbali wameanza kulipwa.
Pia Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kubakia katika mikoa inayolima pamba kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa mauzo ya pamba ili kuhakikisha wakulima wote wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Kuhusu suala la makato ya fedha za pembejeo ambazo wakulima wanalalamikia kukatwa kiasi kikubwa kuliko kiwango halisi wanachostahili, Waziri huyo wa Kilimo amesema atalishughulikia.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Bariadi, Andrew Chenge amesema amefanya ziara katika kata 20 kati ya 30 kwenye jimbo hilo na changamoto kubwa ya wananchi ni mauzo ya pamba. “Ujio wa Waziri Mkuu umeleta manufaa kwani wanunuzi wameanza kuja kwa kasi”.
Mbunge huyo amemuomba Waziri Kuu awafikishie salamu zao kwa Rais Dkt. John Magufuli kwamba wanamshukuru kwa namna anavyowajali wakulima mbalimbali nchini wakiwemo na wa zao la pamba.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Nsangali ambayo inanunua pamba amemuahidi Waziri Mkuu kwamba ifikapo kesho (Ijumaa, Agosti 9, 2019) saa nane mchana atakuwa amelipa sh. milioni 135 zinazohitajika na amcos ya Itemelo ili kulipia deni la pamba iliyoko ghalani.
Awali, Katibu wa Amcos ya Itemelo, Lucas Ephraim alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuyahimiza makampuni mbalimbali yanayonunua yapeleke fedha kwa wakati ili kukidhi makisio tarajiwa.
Katibu huyo alisema chama chao kinahudumia vijiji vitano vikiwa na jumla ya wakulima 2,665 wa pamba wenye jumla ya ekari 9,675. Pia chama chao kinahitaji sh. milioni 135.139 ili kulipia deni la pamba ambayo iko ghalani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwa mkoani Simiyu kwenye shughuli za maadhimisho ya Nanenane. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwa mkoani Simiyu kwenye shughuli za maadhimisho ya Nanenane. |
WAKATI HUO HUO, changamoto ya ucheleweshwaji wa malipo kwa wakulima baada ya kuuza mazao yao inatarajiwa kuwa historia baada ya Serikali kuzindua mfumo wa uuzaji wa Mazao kupitia Soko la Bidhaa (TMX) ambao kuanzia mwaka ujao utaanza kutumika kununua na kuuza baadhi ya mazao ndani na nje ya nchi.
Ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia Soko la Bidhaa unalenga kuongeza ufanisi katika mifumo ya masoko ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu kwa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa, kuleta ushindani kwenye bei, kupunguza gharama na kuweka uwazi.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanywa Agosti 8, 2019 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya maonesho Nyakabindi mkoani Simiyu kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu amesema mfumo huo utawahakikishia wakulima upatikanaji wa malipo kwa muda mfupi na wanunuzi kuwa na uhakika wa kupata mazao na bidhaa zenye ubora na zinazotosheleza mahitaji yao.
“Baadhi ya mazao tunayotarajia kuanza nayo ni pamoja na dengu, choroko, mbaazi, ufuta, korosho, kahawa na kokoa. Mfumo huu utasaidia upatikanaji wa masoko ya uhakika na kwa uwazi na hivyo kuifanya nchi ijulikane kimataifa juu ya uzalishaji wa mazao hayo na mengine”.
Pia, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwenye sekta za kilimo, viwanda na biashara ni lazima soko la bidhaa lipewe ushirikiano kwenye ngazi zote kuanzia Wizara, Mikoa na Halmashauri za Wilaya ili mazao ya kimkakati pamoja na yale yenye changamoto ya masoko yauzwe kupitia soko hilo muhimu.
“Taratibu zote za unedeshaji wa biashara hiyo zikamilike kwa ushirikiano wa vyama vya ushirika, TAMISEMI, Wakala wa Stakabadhi Ghalani na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Fedha na Mipango. “Pia elimu kwa wadau wote itolewe kwa muda wote ili kuwaandaa washiriki wa mnyororo mzima wa thamani za mazao”.
Waziri Mkuu amesema Soko la Bidhaa Tanzania ni taasisi iliyoanzishwa na kusimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa ya mwaka 2015 na Kanuni za Masoko ya Bidhaa za mwaka 2016.
“Aidha, napenda kusisitiza kuwa kuanza kufanya kazi kwa mfumo huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ibara namba 22(g)(ii) ya 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17– 2020/21) na Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II)”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezindua mfumo mwinginewa Kielektroniki wa Kusimamia Biashara za Kilimo (Agricultural Trade Management Information System – ATMIS).“Mifumo hii inalenga kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali za kuendeleza sekta za kilimo nchini na kuimarisha biashara ya mazao na bidhaa za kilimo.
Vilevile, Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali inasimamia utekelezaji wa BluePrint inayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. “Kupitia BluePrint hiyo, changamoto mbalimabali zimeainishwa na kuwekewa utaratibu wa kutatuliwa”.
Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni kuwepo kwa mlolongo mrefu wa kupata vibali na leseni za uwekezaji na biashara na wateja kulazimika kufuata vibali hivyo kwenye Ofisi za Taasisi zilizopewa mamlaka ya kutoa leseni na vibali hivyo.
“Niwapongeze Wizara ya Kilimo na Taasisi ya TradeMark East Africa kwa kusanifu na kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutoa vibali, leseni na huduma za malipo kwa wafanyabiashara”.
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo kusimamia utekelezaji wa mfumo huo ili lengo linalotarajiwa na Serikali hususani kurahisisha biashara liweze kufikiwa. Pia, Taasisi na Idara zote zinazotumia mfumo huo zihakikishe zinatoa elimu kwa watumiaji na wadau wote wa mfumo kwa lengo la kuondoa urasimu katika kuwahudumia wateja.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika kutekeleza mkakati wa kuimarisha mfumo wa biashara za mazao nchini Serikali imetengeneza Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji wa leseni, vibali na malipo ya huduma (ATMIS) ili kurahisisha biashara za mazao ya kilimo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Wizara ya Kilimo wahakikishe wanashirikiana na viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara kusimamia mifumo hiyo sanjari na kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema kuwa maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Tasnia ya Ushirika nchini itaimarika baada ya kuzinduliwa mfumo rasmi wa mauzo ya mazao ya kilimo kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Amesema kuwa TMX imeanzishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika juhudi za Serikali za kurasimisha mifumo ya masoko ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu; kwa kuwaunganisha Wauzaji na Wanunuzi wa bidhaa, kuleta ushindani kwenye bei, kupunguza gharama za uendeshaji biashara na kuweka uwazi.
Mbali na soko la bidhaa pia amesema kuwa kuzinduliwa kwa Mfumo wa Kielektoniki wa Kusimamia Biashara (Agricultural Trade Management Information System – ATMIS) utaimarisha makusanyo ya maduhuli na tozo kwa kuhakikisha huduma zote za utoaji vibali, leseni na vyeti unafanyika kielektroniki na pia kudhibiti udanganyifu katika hati na nyaraka za huduma hizo.
Amesema faida zingine ni kuhakikisha kuwa kazi ya kumhudumia mteja inafanyika kwa wakati mara tu baada ya hatua zote za maombi ya utoaji vibali, na vyeti kumalizika. Pia kuimarisha upatikaji wa taarifa na takwimu muhimu za uingizaji na usafirishaji mazao ya kilimo nje ya nchi na Kuondoa tatizo la nyaraka bandia ambalo huchangiwa na matumizi ya mfumo.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Nane Nane ya mwaka huu inasema: - “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.Kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi wa viwanda na biashara, ikilenga kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa na wakati huo huo kupunguza umaskini.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Naibu Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Madini, Stansalaus Nyongo pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
No comments:
Post a Comment