WAZIRI MKUU AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU WA VIET NAM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 13 July 2019

WAZIRI MKUU AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU WA VIET NAM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung, katika mazungumzo ya faragha yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 12, 2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam,Trinh Dinh Dung wakigonganisha glass katika chakula cha mchana alichoandaa Waziri Mkuu wa Tanzania  kwa heshima ya mgeni huyo kwenye hoteli ya Hyatt Regency- Kilimanjaro jijini Dar es salaam, Julai 12, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimkabidhi  zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro, Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung, baada ya mazungumzo yao, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 12, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekuna na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Viet Nam, Trinh Dinh Dung na amewakaribisha wawekezaji kutoka Viet Nam waje kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya mipango miji, madini, bandari, usafiri wa anga, ufundi stadi, kilimo pamoja na uvuvi.

Amesema kuwa anatambua kwamba nchi ya Viet Nam inafanya vema katika suala la mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kwenye mazao hayo na kukifanya kilimo kuwa cha biashara, hivyo amezialika kampuni za Viet Nam zenye teknolojia mahsusi katika maeneo tajwa ili kushirikiana na Tanzania katika mikakati yake ya kuendeleza kilimo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Julai 12, 2019 wakati wa mkutano wake na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam , ambapo ametumia fursa hiyo kumuhakikishia kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Viet Nam kwa manufaa ya watu wa nchi mbili hizo.

Amesema uwepo wa kampuni ya Viettel PLC (Halotel) ya kutoka nchini Viet Nam ni ishara tosha ya imani ya uwekezaji iliyopo kwa wawakilishi wa Viet Nam. “Nawakaribisha sana wawekezaji kutoka Viet Nam kuja kuwekeza Tanzania kwani kwa kufanya hivyo hawatojutia uamuzi wao wa kuwekeza Tanzania.”
Waziri Mkuu amesema Viet Nam imeendelea kuwa mshirika muhimu wa kiuchumi kwa Tanzania, hivyo ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Viet Nam kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Kwa mfano, kampuni ya mawasiliano ya Viettel PLC (maarufu kama Halotel) ambayo imewekeza nchini tangu mwaka 2014 inafanya vizuri katika sekta ya mawasiliano. Kampuni hiyo, imewezesha mawasiliano ya simu kuwafikia Watanzania wengi hususan wale waishio vijijini.”

Waziri Mkuu amesema kampuni hiyo ya Halotel imeweza kuzalisha ajira takriban 1,600 za moja kwa moja kwa wazawa na ajira takriban 100,000 zisizokuwa za moja kwa moja hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018;
Amesema lengo la Serikali ya Tanzania ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Viet Nam katika masuala ya mawasiliano na masuala mengine ikiwemo biashara na uendelezaji na masoko ya mazao ya kilimo hususan korosho, kahawa, kilimo mseto cha mpunga na uvuvi wa samaki ambako Viet Nam inafanya vizuri zaidi.
Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Waziri Mkuu amesema Tanzania ni nchi nzuri, watu wake ni wakarimu na pia imebarikiwa vivutio vingi vya utalii. Hivyo, amezikaribisha kampuni za Viet Nam kuja kuwekeza katika sekta ya utalii na utamaduni nchini.
“Halikadhalika, sina shaka kwamba wengi wenu mmewahi kusikia kuhusu Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, pamoja na Mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Hivyo ni baadhi tu ya vivutio vingi vya utalii tulivyojaliwa kuwa navyo nchini mwetu.” 
Kwa upande wakeNaibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam, Trinh Dinh Dung ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushgirikiano na kwamba ameomba ushirikiano huo uimarishwe kupitia ziara za viongozi wa wakuu wa nchi mbili hizo.
Naibu Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam, amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba Serikali ya Viet Nam itazidi kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania hususani katika sekta za kilimo, biasdhara na uvuvi.
Kadhalika kiongozi huyo amesema kuwa nchi ya Viet Nam iko tayari kununua mazao mbalimbali ya kutoka nchini Tanzania yakiwemo ya korosho na pamba. Amesema lengo la Serikali yao ni kuhakikisha kwamba biashara kati ya Tanzania na Viet Nam inafikia dola bilioni moja ifikapo 2020.

No comments:

Post a Comment