Kaimu katibu tawala anayeshughulikia masuala ya Kilimo,Uchumi na uwezeshaji mkoa wa Songwe ,Evance Kakulanga akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la siku tatu kwa wadau wa zao la Alizeti liliofanyika mkaoni Mbeya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) Michael Kirumba akizungumza wakati wa Kongamano hilo la siku tatu.
Washiriki wa kongamano la mafunzo lililoandaliwa na Programu ya kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kongmano hilo lililofanyika mkoani Mbeya.
Na
Dixon Busagaga, Mbeya
MASHARTI ya mikopo yanayotolewa na
taasisi za fedha nchini kwa ajili ya wakulima yanatajwa kuwa kikwazo kwa baadhi
ya wakulima wa zao la Alizeti nchini kushindwa kufanya kilimo chenye tija kwa
zao hilo.
Moja ya Masharti hayo ni pamoja na
wakulima kujiunga katika vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo jambo
ambalo wakulima wengi wa Alizeti wameshindwa kutumiza sharti hilo kutokana na
kuamua kufanya shughuli za kilimo bila ya kuwa kwenye kikundi.
Kutokana na hali hiyo tayari
Wakulima wa zao la Alizeti nchini wameshauriwa kujiunga katika vikundi ikiwa ni
pamoja na kuanzisha vyama vya ushirika ambavyo vitasaidia katika kuanzisha
mchakato wa kupata mikopo pamoja na pembejeo za kilimo kwa ajili ya zao hilo.
Ushauri huo umetolewa wakati wa
Kongamano la mafunzo liloandaliwa na Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya
Kilimo Tanzanina (AMDT), kongamano lililofanyika mkoani Mbeya likiwahusisha
wadau mbalimbali wa zao la Alizeti kutoka mikoa 16 ya Tanzania bara.
Wakati wa mijadala katika kongamano
hilo baadhi ya wakulima na wadau wa zao la Alizeti walisema kumekuwepo na
changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, hali ambayo wameitaja kuwa ni
kikwazo katika kumsaidia mkulima mdogo wa zao hilo.
“Ni ukweli usiopingika wengi wetu
licha ya kuvutiwa na kilimo cha Alizeti, kutokana na hamasa na elimu ambayo
tumekuwa tukiipata kutoka kwa wadau wetu wa kilimo lakini tunashindwa kufanya
kilimo chenye tija kutokana na uwezo wetu kuwa mdogo” alisema Anita Mwakyoma
ambaye ni msindikaji wa mafuta ya Alizeti.
Alisema pamoja na ugumu wa
upatikanaji wa mikopo, bado wakulima wengi wameshindwa kumudu bei za mbegu bora
za Alizeti zinazopatikana sokoni na hivyo kulazimika kutumia mbegu zisizokuwa
na ubora ambazo zimekuwa hazitoi mbegu za kutosha hali ambayo inayomfanya
mkulima asinufaike na kilimo.
“Pamekuwepo na jitihada kubwa sana
inayofanya na wadau wa kilimo na hasa maafisa ugani katika kutuhamasisha juu ya
umuhimu wa matumizi ya mbegu bora ambazo hutoa mazao mengi wakati wa mavuno,
lakini kutokana na gharama kubwa ya mbegu hizi wengi wetu tunashindwa.”alisema
Mwakyoma.
Naye Mkulima wa Alizeti katika mkoa
wa Songwe Sophia Mwanandenga aliziomba mamlaka zinazohusika na Kilimo hususani
upande wa Pembejeo kuangalia namna zitakavyomsaidia mkulima kupata mbegu bora
kwa bei nafuu.
Akijibu hoja ya upatikanaji wa
mikopo kwa wakulima wadogo, mwakilishi wa Benki ya Posta Nchini Tawi la
Mbeya,Leonard Katamba alisema kwa muda mrefu mkulima mdogo amekuwa
hakopesheki kutokana na kushindwa kufikia vigezo vilivyowekwa na baadhi ya
taasisi za fedha.
“Kwa kutambua mchango wa mkulima
katika ukuaji wa uchumi nchini, TPB tumeanzisha mpango maalumu wa kuwahamasisha
wakulima kujiunga na vikundi, hatua ambayo itakuwa ni msaada kwa mkulima kuweza
kupata mikopo pindi atakapokuwa anahitaji.”alisema Katamba.
“Kwa sasa tunawahamasisha wajiunge
katika vikundi ili waweze kufikiwa kwa urahisi na wadau mbalimbali walioko
katika mnyororo wa thamani wa zao la Alizeti , na tayari tumeanza kuyaona
mafanikio katika maeneo ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Iringa na Mkoa wa
Njombe”aliongeza Katamba .
Alisema katika maeneo hayo tayari
wakulima wamehamasishwa kuanzisha vikundi ambavyo hadi sasa licha ya kusubili
mikopo kutoka benki tayari wameanza utamaduni wa kujiwekea akiba jambo ambalo
linatajwa kma hatua njema.
“Hii kwetu ni hatua nzuri maana kwa kujiwekea
akiba mkulima hata lazimika kuchukua mikopo bila sababu ya msingi maana tayari
wanakuwa na akiba ambayo inaweza kuwasaidia katika hatua mbalimbali wakati wa
kilimo.”alisema Katamba.
Kwa Upande wake mtafiti wa mbegu
kutoka taasisi ya utafiti wa mbegu nchini (TARI) Samweli Mwenda alisema taasisi
yao mpaka sasa inaendelea na tafiti mbalimbali ambazo zimelenga kumsaidia
mkulima kupata mbegu bora na ambayo itakuwa na tija kwa mkulima wa Alizeti
nchini.
“Sisi kama taasisi ya serikali
jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunapata mbegu bora na zenye tija na mpaka sasa
tunaendelea na tafiti mbalimbali ili kuleta mbegu mpya pamoja na kusafisha au
kuboresha mbegu mbalimbali zilizopo sokoni ili mkulima aweze kupata mavuno
mengi na yenye tija. alisema Mwenda.
Naye Meneja wa zao la Alizeti kutoka
taasisi ya Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzanina AMDT,
Martin Mgallah amesema kuwa wao kama taasisi ambayo imekusudia kumuinua mkulima
wa zao la Alizeti nchini itaendelea kwa kushirikiana na wadau wake kuhakikisha
wakulima wanakuwa katika vikundi ili viweze kuwa na sifa ya kukopesheka hatua
ambayo itakuwa ndio mkombozi kwa mkulima.
Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya
Kimasoko Katika Kilimo Tanzania,AMDT imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali
katika mikoa 15 nchi ambapo mpaka sasa zaidi ya wakulima 150,000 wamekwisha
fikiwa kupitia mradi huu ambao lengo lake kubwa ni kumwezesha mkulima mdogo
kupata tija katika kilimo hicho kwa kulima na kuzingatia kanuni bora za kilimo.
No comments:
Post a Comment