Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi- CCM, Dkt. Bashiru Ally, akieleza umuhimu wa elimu katika maendeleo ya jamii, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Qur'an Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma. |
Mtoto Summayya Juma, akionesha uwezo wake wa kuhifadhi Qur'an katika mashindano yaliyofanyika Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma. |
Na Peter Haule, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi- CCM Dk. Bashiru Ally, amewataka watanzania kutumia uwezo wa kuhifadhi Vitabu vitakatifu kuongeza ubunifu katika nyanja ya Sayansi na Teknolojia na nyingine ili kuendeleza jamii kwa kuipatia maendeleo stahiki.
Dkt. Bashiru ametoa wito huo katika Kata ya Pahi wilayani Kondoa mkoani Dodoma, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Qur'an yaliyowashirikisha wadau kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa katika kuwekeza kwenye elimu kwa watoto, kwa kuwa watoto wakisoma si tu wanajengewa maarifa lakini pia wanaunganishwa na hivyo kuwa chachu ya kuweza kuisaidia jamii inayowazunguka.
Mratibu na Mwandaaji wa mashindano hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa lengo la mashindano hayo ya kuibua vipaji vya watoto vya kusoma Kitabu Kitukufu cha Qur'an na kuwajengea vijana uwezo wa kuwa na ujasili katika kueleza wanayo yaamini yakiwemo mambo mazuri ambayo yanafanywa na Serikali.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, alisema kuwa kazi zinazofanywa na Dkt. Ashatu Kijaji, ni zakupigiwa mfano hasa kwa wanawake na akawataka wazazi katika Wilaya ya Kondoa kumuunga mkono kwa kushiriki kikamilifu katika mikakati ya kuinua elimu katika eneo hilo, kwa kuhakikisha wanawapeleka watoto katika makambi yaliyo na lengo la kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Mgeni Rasmi katika Mashindano hayo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapher Shabaan, amewapongeza vijana walioshiriki mashindano hayo na kuonesha umahili mkubwa wa kuhifadhi Qur'an na kuwataka waumini wa kiislamu kusoma na kukielewa kitabu hicho kitukufu kwa kuwa kimejaa elimu na maarifa mengi yatakayo wasaidia kuenenda vyema katika jamii na kupata thawabu kutoka kwa Mungu.
No comments:
Post a Comment