Waziri wa Nishati
Dkt. Medard Kalemani akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara
hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Leo Bungeni Jijini Dodoma.
Mbunge wa Muleba Kusini Mhe. Charles Mwijage akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2019/2020 leo Bungeni Jijini Dodoma. |
Na
Mwandishi Wetu
WIZARA ya Nishati
yaomba Kuidhinishiwa Shilingi Trilioni 2.142 ikilinganishwa na shilingi
Trilioni 1.692 iliyotengwa kwa mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia
26.6 kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme.
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Medard
Kalemani amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na kuanza kutekelezwa kwa mradi
mkubwa wa Rufiji utakaozalisha megawati 2,115 utakapokamilika.
“Fedha nyingi za
ndani za miardi ya maendeleo zilizotengwa kwa mwaka 2019/2020 zimeelekezwa
katika miradi mitatu ya kimkakati ambazo ni shilingi trilioni 1.86 sawa na
asilimia95.1 ya bajeti yote ya ndani,” Alisisitiza Dkt. Kalemani.
Akifafanua Dkt.
Kalemani amesema kuwa miradi hiyo ni; Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Mto Rufiji MW
2,115 uliotengewa shilingi Trilioni 1.44, Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme
Vijijini Awamu ya Tatu Shilingi Bilioni 363.11 na Mradi wa Kuzalisha Umeme wa
Kinyerezi 1 Extension MW 185 shilingI
Bilioni 60.
Aliongeza kuwa Bajeti
ya mwaka 2019/2020 inalenga kutekeleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kuhakikisha kuwa inazalisha umeme wa kutosha, wa uhakikka, unaotabirika na
wenye gharama nafuu.
Vilevile, Bajeti hiyo
imelenga kuimarisha shughuli za utafutaji na biashara ya mafuta na gesi asilia
pamoja na kuwezesha wananchi kunufaika na rasilimali hizo. Lengo jingine ni
kuwezesha ujenzi wa uchumi wa Viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025 hali itakayosaidia kujenga uchumi jumuishi na kuinua kiwango cha maisha ya
wananchi wote hasa wale wanaoishi vijijini.
Akizungumzia
upatikanaji wa mafuta hapa nchini Dkt. Kalemani amesema kuwa imeendelea
kuimarika kupitia utaratibu wa Serikali kuagiza mafuta kwa pamoja kupitia
Wakala wa uagizaji Mafuta kwa pamoja.
“ Kati ya mwezi
Januari hadi Desemba, 2018 jumla ya lita Bilioni 5.70 za mafuta zilizgizwa
kupitia Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara sawa na ongezeko la asilimia
6.3 ikilinganishwa na lita Bilioni 5.36 zilizoagizwa mwaka 2017” Alisisitiza
Dkt. Kalemani.
Kwa upande wa
usambazaji wa gesi asilia Dkt. Kalemani amesema kuwa wateja 500 wameunganishiwa
huduma hiyo katika Jiji la Dar es Salaam hali itakayosaidia kupunguza gharama
za maisha kwa wananchi wote watakaoungnishiwa huduma hiyo.
Akizungumzia hatua
iliyofikiwa katika kuunganisha viwanda na huduma ya gesi asilia amesema kuwa
zoezi hilo linaendelea na viwanda kadhaa vimeshaunganishiwa. Kwa upande wa makisio
ya makusanyo ya maduhuli kwa mwaka 2019/2020 yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni
602.05 sawa na ongezeko la asilimia 52.6 ikilinganishwa na shilingi Bilioni
394.45 lililokuwa lengo la mwaka 2018/19. Ongezeko la makisio ya makusanyo
limetokana na kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali gesi asilia.
Wizara ya Nishati imeomba
Kuidhinishiwa Shilingi Trilioni 2.142 na Bunge ikilinganishwa na shilingi
Trilioni 1.692 iliyotengwa kwa mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia
26.6 kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
No comments:
Post a Comment