Almasi |
Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imetajwa
kuweka historia katika tasnia ya madini baada ya Almasi yenye Karati 512.15
kupatikana hivi karibuni katika eneo la Maganzo Mkoani Shinyanga na kuuzwa kwa jumla ya shilingi Bilioni 3.2.
Akizungumza katika
mahojiano maalum kuhusiana na madini hayo,Naibu
Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa kutokana na
kupatikana kwa almasi hiyo Serikali itapata mapato ya takribani shilingi milioni 235,000/- kama kodi na tozo
mbalimbali ikiwemo mrabaha ambayo yamelipwa Serikalini baada ya mauzo hayo.
Kuuzwa kwa jiwe hilo
moja la almasi katika soko la madini mkoani Shinyanga ni muendelezo wa tija
inayopatikana kupitia masoko hayo toka kuanzishwa kwake nchini, jumla ya
shilingi bilioni 34.3 zimepatikana kwenye biashara ya dhahabu iliyofanyika
katika kipindi cha mwezi mmoja tu kati ya Machi 17 mpaka Aprili 17 mwaka huu
katika masoko ya madini kote nchini, kwa mujibu waziri wa Madini, Doto Biteko, aliyetoa
taarifa hiyo hivi karibuni.
“Natoa wito kwa
wachimbaji wote,madalali na mawakala, kuyatumia ipasavyo masoko hayo kwakuwa
kila mmoja atapata stahiki yake tofauti na awali kabla ya kufunguliwa kwa
masoko hayo ambapo wachimbaji hawakuwa kwenye mikono salama kufutia kutokuwa na
mfumo rasmi wa uuzaji madini yao”. Alisisitiza mhe. Nyongo.
Akifafanua amesema
kuwa kila mchimbaji anapaswa kuzingatia sheria na Kanuni za sekta ya madini ili
kuepuka mkono wa sheria na hatua nyingine ikiwa ni pamoja na kutaifishwa kwa
madini yao pale watakapobainika kutaka kutorosha madini ama kujihusisha na
magendo.
Aliongeza kuwa baada
ya kupatikana kwa almasi hiyo wataalamu wa Wizara hiyo walifanya tathmini ili
kuona ubora wake na kiwango kilichopatikana ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata
mapato yake.
“ Serikali ya Awamu
ya Tano imeweka makazo katika kuimarisha sekta ya madini nchini ili itoe
mchango unaostahili katika uchumi wetu ndio maana tunaona kuwa kupitia masoko
ya madini tuliyoanzisha hata mchimbaji huyu aliyepata hii almasi pale Maganzo
aliiuza kupitia soko letu la madini baada ya kufuata taratibu zote” alisisitiza
Mhe. Nyongo
Tanzani ni moja ya
nchi zenye utajiri mkubwa wa madini ya aina mbalimbali ikiwemo Almasi,
Tanzanite, Dhahabu na mengine mengi. Serikali ya Awamu ya
Tano imeweka mkazo katika kuimarisha sekta ya madini ikiwemo kuimarisha
taratibu za uuzaji wa madini yote yanayozalishwa hapa nchini, kuimarisha
usimamizi, kuwawezsha wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba kwa tija.
No comments:
Post a Comment