TMA YATOA AGALIZO KUTOKANA NA MVUA ZINAZOENDELEA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 11 May 2019

TMA YATOA AGALIZO KUTOKANA NA MVUA ZINAZOENDELEA

Baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam barabarani yakiwa yamejaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa mwenendo wa hali ya hewa hususan mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo hapa nchini, huku akitoa angalizo kwa wananchi.

Taarifa kwa umma imesema mvua zinazoendelea kunyesha nchini hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki na kanda ya ziwa Victoria ni sehemu ya mvua za Masika, ambazo zinatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua (ITCZ).

"Mvua za mfululizo katika baadhi ya maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es salaam na Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) zinatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha siku mbili zijazo (mpaka siku ya Jumapili tarehe 12 Mei 2019).

Aidha vipindi vya mvua za mfululizo vinatarajiwa kujirudia kuanzia katikati ya mwezi Mei, 2019. Mamlaka itatoa taarifa za mara kwa mara za mwenendo wa mvua hizo katika taarifa zake za utabiri," imesema taarifa hiyo.

ANGALIZO: Pamoja na kwamba mvua za masika zinatarajiwa kupungua katika maeneo mengi mwishoni mwa mwezi Mei, 2019; athari za mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi cha wiki moja mfululizo katika ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba zimesababisha kutuama kwa maji na mafuriko. Hivyo kutokana na ardhi kuwa na unyevunyevu mwingi, ongezeko kidogo la mvua linaweza kuendelea kusababisha athari kama zilizokwisha jitokeza.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na
kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Imetolewa tarehe 10 Mei 2019 na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

No comments:

Post a Comment