Mch. Ezekia Majani, akijiandaa kubatiza waumini waliokubali Yesu. |
Baadhi ya Wachugaji wakichangia jambo kwenye mkutano wa pamoja. |
Baadhi ya wachungaji walipofanya ziara ya kuwatembelea wahitaji na wenye shida mbalimbali katika Kijiji cha Kalulu. |
Baadhi ya wachungaji walipofanya ziara ya kuwatembelea wahitaji na wenye shida mbalimbali katika Kijiji cha Kalulu. |
Baadhi ya Wachugaji wakiwa katika picha kwenye ziara hiyo. |
Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA). |
Na Adam Mwambapa, Tunduru
JOPO la wanafunzi wapatao 30 kutoka Chuo Kikuu TEKU kilichopo jijini Mbeya, wameigusa mboni ya Mungu moja kwa moja Ijumaa hii, pale walipofanya ziara ya kuwatembelea wahitaji na wenye shida mbalimbali katika Kijiji cha Kalulu.
Kijiji kilichopo tarafa ya Kalulu, kata ya Matemanga, wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Tendo hili lililofanywa na wanafunzi wa Kitivo cha Theolojia, halijawashangaza tu wakazi wa Kalulu, isipokuwa limewaacha midomo wazi wakazi wa wilaya nzima ya Tunduru kwani ni mara ya kwanza.
Huu ndiyo upendo wa kweli alioutangaza Yesu kwa watu wote, aliotumwa na Mungu aueneze ulimwenguni, sawasawa na Neno lisemalo: “Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu,” (Yakobo 1:27).
Akizungumza katika tukio la kuwagawia wakazi wa eneo hilo misaada ya nguo, mara baada ya huduma ya Neno la Mungu kupita, Mhadhiri wa TEKU ambaye pia ni mlezi wa wanafunzi hao, Mchungaji Ezekia Majani, alisema:
“Lengo kuu ni kuwafanyia watu Uinjilisti wale wasiomjua Yesu, na wale wanaomjua kuwaimarisha kiroho. Wakati lengo kubwa la Ujilisti ni kuwaleta watu kwa Yesu…kwa kuwa, Uinjilisti ni ushawishi,”alisema Mchungaji Majani.
Akiendelea kueleza Mchungaji Majani alisema, tumechagua kuja Tunduru kwa sababu ya changamoto iliyopo ya kumjua Kristo, tofauti na maeneo mengine.
“Kimsingi, Tunduru na wilaya zingine za kusini asilimia Zaidi ya 80 ni Waislamu. Wakati asilimia zilizosalia ndiyo Wakristo, sasa utaona kabisa uhitaji wa kuinjilisha ulivyo eneo hili,”alisema.
Utafiti unaoonesha kuwa, mikoa ya kusini kama Lindi na Mtwara pamoja na wilaya zake. Imechelewa sana kupata maendeleo ya huduma nyingi za kijamii, kwa sababu tu waliukataa Umissionari kwa nguvu zote; hata inasemekana kuwa Mmissionari wa kwanza kuja Tunduru aliuawa kwa kifo cha kutisha.
Naye Mwenyekiti wa Wanafunzi wa TEKU, Mchungaji Afwilile Mwankuga, alisema, ili mtu akue na kumjua Mungu kisawasawa ni lazima apate huduma ya kimwili na kiroho.
“Tunamtegemea mwanadamu ili akue basi ni shurti aipate huduma ya kimwili ambayo ni mavazi, lakini aipate pia huduma ya kiroho ambayo ni kumjua Mungu mwenyewe kiundani,”alisema Mch. Mwankuga.
Aidha, Mchungaji Mwankuga, kwa kukazia zaidi hoja hiyo ya kumtambua Mungu, aliendelea kusema:
“Kwa kawaida huwezi kuzitenganisha huduma hizi mbili kwa namna yoyote ile. huduma hizi zinategemeana kwa kiasi kikubwa sana na ndivyo Mungu anavyotutaka kuzitenda,”alisema.
Sultani (Mwenye) Mpelembe wa kabila la Wayao, ni miongoni mwa mamia waliohudhuria mkutano huo wa Injili uliofanywa na TEKU. Hakusita kuisifia huduma iliyofanyika huku akiwa na haya:
“Nashukuru kufanyika mkutano na kuisha salama, licha ya kwamba huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu na wengi wako kwenye mfungo.”
Mkutano huo ni wa siku mbili, ambapo unatarajiwa kuhitimishwa Jumapili hii kwenye Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA), Kanisa ambalo ni mshirika wa TEKU na limo kwenye Umoja wa Maknisa (CCT). Lililopo Kijiji cha Milonde, kata ya Matemanga wilayani Tunduru.
No comments:
Post a Comment