Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe Mhandisi Izack Kamwelwe (katikati) akitoa maelekezo kwa watendaji wake kwenye hafla hiyo. |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dk. John Pombe Magufuli ameomba kuandaliwa orodha ya maofisa wakuu Serikalini 'vigogo' ambao wanatumia line za Shirika la Mawasiliano Tanzania, TTCL Corporation, ili kubaini ni wapi ambao sio wazalendo na hawalitumii line hizo kuliunga mkono shirika hilo.
Rais Dk. Magufuli ametoa agizo hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba jana alipokuwa akipokea Gawio la Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 2.1 toka TTCL jijini Dar es Salaam.
Dk. Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhimiza uzalendo kwa Watanzania kwa masuala mbalimbali ya msingi yanaloligusa taifa, alilazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kuona ni taasisi chache za umma ambazo zinatumia huduma za TTCL Corporation, ambalo ni shirika la Watanzania wote.
"Naomba mniandalie orodha ya maofisa wa juu ambao wanatumia huduma za TTCL ili nianze na hawa...ambao Serikali inawalipa mshahara na hawaliungi mkono shirika lao la simu la kizalendo kwa kutumia huduma zake. Watanzania lazima tuwe wazalendo kwa kupenda na kujivunia vyakwetu, sisemi msitumie kampuni zingine hapana lakini kwani ukiwa mteja kote kote (mtandao zaidi ya mmoja) kuna ubaya gani," alisisitiza Rais Dk. Magufuli.
Alisema faida inayopatikana kwenye huduma za TTCL Corporation inarudi serikalini na kusaidia huduma mbalimbali za maendeleo hivyo kila Mtanzania mzalendo anawajibu wa kuliunga mkono shirika hilo ili liweze kutengeneza faida zaidi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Awali kabla ya kukabidhi gawio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Kindamba alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18 Shirika hilo liliendelea kupata mafanikio katika majukumu yake ya kutoa huduma za mawasiliano na kusimamia na kuendesha miundombinu mkakati ya mawasiliano ambapo Shirika limepata faida baada ya kutoa kodi ya shilingi bilioni 8.3.
"Faida hii imetokana na shirika kupata mapato ya shilingi bilioni 119.4 wakati jumla ya matumizi na kodi kwa mwaka ni shilingi bilioni 111.1. Kutokana na mafanikio hayo, Shirika linatoa gawio la shilingi bilioni 2.1 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiye Mwekezaji pekee katika Shirika hili. Gawio la mwaka huu ni ongezeko la Tsh Milioni 600 kutoka katika Gawio la Tsh Bilioni 1.5 tulilotoa mwaka jana," alibainisha Bw. Kindamba.
Aidha alizitaja Wizara za Serikali na Mashirika ya huduma muhimu za Kijamii ambayo yanatumia huduma za TTCL kuwa ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Tanesco, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Tume ya Vyuo Vikuu, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Hospitali za rufaa Nchini na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment