MWILI WA DK. MENGI WAWASILI DAR, WANANCHI WAMPOKEA 'KIFALME' - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 6 May 2019

MWILI WA DK. MENGI WAWASILI DAR, WANANCHI WAMPOKEA 'KIFALME'

Jeneza lenye mwili wa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi likiingizwa kwenye gari tayari kwa safari.
Na Joachim Mushi, Dar

MWILI wa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi umewasili leo jijini Dar es Salaam kwa ndege ukitokea jijini Dubain Uarabuni ambapo umauti ulimkuta.

Mwili huo uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julias Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam majira ya saa tisa alasiri na kupokewa na viongozi mbalimbali, mamia ya wananchi wakiongozwa na wanafamilia, mkewe pamoja na watoto wake.

Mwili wa Dk. Mengi baada ya kupokewa ulianza safari kuelekea kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ambapo ulipitishwa baadhi ya maeneo barabarani na kuvuta hisia za wananchi wengi waliojitokeza kutoa pole.

Ukiwa njiani ukitokea Uwanja wa Ndege barabarani baadhi ya wananchi makundi mwalimbali walikimbilia gari lililobeba mwili wa Dk. Mengi na kuligusa huku wengine wakilirushia maua na majani kwa ishara ya kumuaga.

Maeneo ya Buguruni, Ilala, Kigogo, Magomeni, Kinondoni, Victoria, Mwenge wananchi waliongezeka kuuaga mwili wa mpendwa wao ambapo magari ya msafara wake yalilazimika kusimama kutokana na idadi kubwa ya waombolezaji waliokuwa wakikimbilia kugusa, kushika na wengine kusukuma gari la mwili.

Wengine walisikika wakilia na kunga matawi ya majani ikiwa ni kuoneshwa kuguswa na msiba huo wa Dk. Mengi kipenzi cha watu wenye ulemavu na makundi mengine.

Magari ya polisi yakiwa na askari katika msafara huo yalionekana kupata changamoto baadhi ya maeneo baada ya kukumbana na makundi ya waombolezaji barabarani wengine wakifunga barabara ilimradi kufanikiwa kuona jeneza la mwili wa kiongozi huyo.

Mwili wa marehemu Dk. Mengi kesho unatarajiwa kuagwa katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza safari kuelekea Mkoa wa Kilimanjaro kwa mazishi, yatakayofanyika Machame.

No comments:

Post a Comment