Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (Afya), Dk. Dorothy Gwajima akiongea na wajumbe wa kamati za usimamizi huduma za Afya mkoa na wilaya za Namtumbo, Songea na Songea Manispaa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (Afya) Dk. Dorothy Gwajima wa kwanza kulia akiongea na ndugu wa wagonjwa kusikiliza kero zao alipotembelea na kukagua kituo cha Afya Mjimwema Manispaa ya Songea. |
Agizo
hilo limetolewa jana mjini Songea na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dk. Dorothy Gwajima
wakati akizungumza na wajumbe wa kamati
ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Mkoa wa Ruvuma pamoja za Halmashauri za wilaya
ya Namtumbo na Songea pamoja na Manispaa
ya Songea.
Amesema
anawapa siku 30 Waganga wakuu wa Mikoa yote kuhakikisha kuwa wanafanya tathmini
ya wajumbe waliopo katika ofisi zao kama wanatosha kuendelea na nyadhifa zao za
kusimamia jukumu la uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zao.
Dk. Gwajima ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hizo
hawana sifa zinazowafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya usimamizi na
uendeshaji huduma za afya katika maeneo yao, waganga wakuu wa mikoa
watalazimika kuwaweka pembeni wajumbe hao na kuunda upya kamati ambazo zitaweza
kuiendeleza agenda ya mabadiliko katika sekta ya afya.
“Kinyume
na hapo katika ziara hizi ninazoendelea kuzifanya mikoani nikikuta yupo Mganga
Mkuu ambaye ametulia tu, mapungufu katika vituo bado yapo na amewezeshwa na
serikali, ajue wazi kuwa wa kutoka wa kwanza atakuwa yeye,” amesema Dk. Gwajima na kuongeza:
“Haiwezekani
tukute mapungufu madogo kabisa katika vituo, ambayo yangeweza kuonwa na wao
walioko huko eti hayaonekani hadi tuje sisi kutoka Tamisemi ndiyo mapungufu hao
yafanyiwe kazi,” amesisitiza Dk. Gwajima.
Naibu
Katibu Mkuu huyo ameonya tabia iliyojengeka miongoni mwa wajumbe wa kamati za
uendeshaji huduma ya afya kukimbilia kuomba msamaha pindi zinaposhindwa
kutekeleza majukumu yake kwa makusudi.
Amesema
huu ni wakati wa kuboresha sekta ya afya katika vituo vya afya na zahanati kwa
kuhakikisha kuwa mazingira ya utoaji huduma yanaboreshwa ili yaweze kuwavutia
wananchi wengi kukimbilia kupata huduma katika zahanati na vituo vya afya
vinavyomilikiwa na serikali.
Dk. Gwajima amesema kuwa kamwe hatawapa nafasi wajumbe wa kamati za uendeshaji
huduma za afya wa mikoa na wilaya ambao siku zote wamekuwa ni watu wa
visingizio vya kuomba kusamehewa ama kupewa muda kuwa wamefahamu mapungufu yao.
Amesema
angependa kuona kamati za uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zikijikita katika
kuongelea mambo makubwa yanayolenga kuishirikisha sekta na serikali kuu.
“Hivi
vitu vidogo vidogo vya kitaalamu tubebe sisi wenyewe, wananchi wametuunga
mkono, tumeweza kushirikiana nao kujenga zahanati na vituo vya afya katika mikoa
na halmashauri zetu hivyo ni jukumu letu sasa kuhakikisha kuwa tunatoa huduma
bora za afya kwa wananchi,” amesema.
Kwa
mujibu wa Dk. Gwajima, katika ziara zake alizokwisha zifanya katika mikoa ya Morogoro,
Dodoma, Njombe na Ruvuma amejionea mapungufu mbalimbali ya utoaji wa huduma
bora za afya katika vituo vya afya na zahanati.
Ameongeza
kuwa mapungufu hayo ambayo ameyashuhudia kwenye vituo vya afya na zahanati
zinazomilikiwa na umma yametokana na watendaji hao kutopata usimamizi unaostahili kutoka kwa
kamati za usimamizi na uendeshaji wa huduma
za afya za mikoa na halmashauri husika.
Dk. Gwajima anaamini kuwa kushindwa kwa kamati za uendeshaji ndiko kulikopelekea
kukithiri kwa uchafu katika majengo ya vituo vya afya na zahanati nchini licha
ya vituo hivyo kuwa na fedha za uendeshaji wake.
Sambamba
na kuwataka waganga wakuu wa mikoa kuzitathmini kamati hizo, Dk. Gwajima
amewataka waganga wakuu wote kutambua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli ana agenda moja tu ya kuleta mabadiliko katika sekta ya
afya.
“Hatutapimwa kwa idadi ya semina au vituo vya
afya tulivyojenga bali kwa ubora wa kazi za kuhudumia wananchi,” amesema.
Dk. Gwajima amebainisha mapungufu kadhaa aliyoyaona kwenye ziara yake kuwa ni
pamoja kuwepo kwa malalamiko toka kwa wagonjwa na kukosekana kwa takwimu sahihi za utendaji kazi.
Akiwa
katika kituo cha afya Mjimwema Manispaa ya Songea Naibu Katibu Mkuu Dk. Gwajima
alipokea kero za wagonjwa kuhusu uwepo wa kauli mbaya toka kwa wauguzi na tatizo
la ukosefu dawa hususan akina mama
wajawazito
“Hapa
Mjimwema nimebaini kasoro nyingi mojawapo kauli mbaya za watumishi na tatizo la
dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa ” Dk. Gwajima alionya.
Kwa
upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk. Jairy Khanga ameahidi kuchukua hatua za mapema kufanya mabadiliko ya
utendaji kazi wa kamati za usimamizi wa huduma za afya katika mkoa wa Ruvuma .
No comments:
Post a Comment