MIJADALA SULUHU YA BIASHARA KUKUA KUPITIA SEKTA YA KILIMO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 27 May 2019

MIJADALA SULUHU YA BIASHARA KUKUA KUPITIA SEKTA YA KILIMO

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akizungumza  wakati wa kongamano lililoandaliwa na Programu ya kuendeleza mifumo ya kimasoko ya kilimo (AMDT), lililowakutanisha wataalamu kutoka sekta binafsi na sekta ya umma wakiwemo Wakuu wa wilaya, Makatibu tawala, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi na Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Nyanda za juu kusini.

Baadhi ya Wakuu wa wilaya kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika kongamano hilo lililofanyika mkoani Mbeya.

 Mkuu wa kitengo cha uboreshaji Mazingira ya Biashara wa Programu ya kuendeleza mifumo ya kimasoko ya kilimo nchini (ADMT), Tertula Swai akizungumza wakati wa kongamano hilo. 

Baadhi ya washiriki katika kongamano hilo kutoka taasisi za Binafsi na zile za umma.

Mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Juma Abdalah akichangia jambo wakati wa kongamano hilo.

Kaimu katibu tawala Mkoa wa Mbeya, Said Madito akizungumza wakati wa kongamano hilo.

Washiriki katika Kongammano hilo wakifuatilia mijadala.

Baadhi ya Wakuu wa wilaya walioshiriki kongamao hilo wakichangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwa lengo la kusaidia sekta ya Kilimo nchini.

  Washiriki wa Kongamano lililolenga majadiliano ya namna ya kuboresha biashara kupitia mijadala ya pamoja baina ya sekta binafsi na watendaji wa vyombo  vya Serikali wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Na Dixon Busagaga, Mbeya


BAADHI ya Changamoto zinazotajwa kuwakabili wafanyabiashara waliopo kwenye Mnyororo wa thamani unatokanana Kilimo ni pamoja na kukosekana kwa mijadala baina ya sekta Binafsi na sekta ya umma kujadili sera, kanuni na miongozo inayoweza kuleta maendeleo katika Biashara kupitia Kilimo.


Katika kuondoa changamaoto hiyo, Programu ya kuendeleza mifumo ya kimasoko ya kilimo (AMDT) umezikutanisha pande hizi mbili jijini Mbeya, sekta binafsi na sekta ya umma wakiwemo Wakuu wa wilaya, Makatibu tawala, Wenyeviti wa Halmashauri ,Wakurugenzi na Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Nyanda za juu kusini.


Lengo la kukutanishwa kwa watendaji hawa wa serikali na wale wa sekta binafsi ni pamoja kuinua maisha ya Mtu, kina Mama kina Baba, Vijana ambao ni maskini kupitia uboreshaji wa mazao ya biashara kwa wakulima, wasindikaji, wasafirishaji wanaofanya kazi katika maeneo ya vijijini.


Mkuu wa kitengo cha uboreshaji Mazingira ya Biashara wa Programu ya kuendeleza mifumo ya kimasoko ya kilimo nchini (ADMT), Tertula Swai alisema kupitia mijadala kwa kiasi kikubwa itachangia kuboresha mazingira ya Biashara.


“Kuna namna mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara moja wapo ni namna ambavyo sekta binafsi na sekta ya Umma wanakaa kwa pamoja wanajadili zile sera mbalimbali, kanuni, miongozo ambayo inaweza kuleteleza maendeleo katika biashara ambazo zinafanyika katika sekta hiyo ya Kilimo,” alisema Swai.


“Kwa nini mjadala ni muhimu, mjadala ni muhimu kwa sababu inawezekana kabisa kwamba katika kufanya biashara aidha ya Kulima, Kuzalisha, Kusafirisha ama Kusindika kuna changamoto ambazo ni kikwazo kwa zile biashara kukua,”aliongeza Swai.


Alisema Serikali wajibu wake ni kuweka mazingira mazuri ya biashara na kwamba pale ambapo kuna changamoto au kuna kikwazo ni wajibu wa serikali kuboresha yale mazingira ili wahusika iwe rashisi kufikia malengo.


“Lakini haya mazingira hayawezi kutokea tu hivi hivi ni lazima sekta binafsi wajadili, wakae pamoja na sekta ya umma kuangalia ni sera zipi hizo, kwa nini ni kikwazo, ni watu wangapi wanaathirika ama wanaumizwa na hizo sera na je zitarekekebishwa vipi.” alisema Swai.



“Yaani sekta binafsi washirikiane na serikali kuja na namna ya kuboresha  na mwisho wa siku wafanyabiashara watafaidika na biashara zao zitakuwa lakini pia serikali itafaidika kwa maana ya kwamba itaongeza mapato”aliomgeza Swai .


Swai alisema Lengo kuu kwa AMDT ni kuongeza kipato  na fursa za ajira kwa Watanzania wa rika lote hususani walioko maeneo ya vijijini na kwamba kupitia program hiyo AMDT inatengeneza mifumo ya masoko. 


“Tunazungumzia mfumo wa uzalishaji mbegu au mfumo wa uuzaji pembejeo au mfumo wa utoaji huduma lakini pia kwenda kuboresha pale ambako kuna upungufu, tukilenga zaidi kwenye mazao ya Mahindi, Mikunde na Alizeti,” alisema Swai


Katika kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Usungulo jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alisema ipo haja kwa Serikali kufanya marekebisho ya sheria za tozo za kodi ili kuwa na tija na rafiki  kwa wakulima na wafanyabiashara.



Kauli ya Chalamila inatokana na uwepo wa changamoto katika eneo la tozo katika ununuzi na usafirishaji wa mazao zinazotajwa kama kero kwa wakulima kupitia mnyororo wa thamani kwa mazao ya Mahindi, Alizeti na Mikunde.



 “Maboresho ya mifumo ya kodi haikwepeki, tusikwepe kuzungumzia maboresho ya mifumo ya kodi, nina amini tukifanya maboresho ya mifumo ya sheria za kodi zetu  maana mifumo yetu ya kodi ya sasa ni ile ya tangu miaka 1990.



Alisema endapo maboresho yatafanyika kwa kiasi itawezesha mifumo kuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wakulima kufanya biashara nchini hatua itakayochangia kuondoa udanganyifu .



Mbali na hilo, Chalamila alisema bado kuna kasumba watu kuzungumza zaidi kuliko vitendo kwenye masuala ya msingi jambo ambalo linakwamisha juhudi za wananchi kama vile wakulima kuhamasisha kulima kwa wingi lakini mwisho wa siku wanakosa masoko na mazao yao kuharibika.



Alisema ‘Tunapohamasisha kitu fulani, ili wenzetu walioko kwenye hali ya kawaida ambao ndio walengwa wakuu maana tunapozungumzia mahindi, alizeti au maharage, utagundua kwamba Watanzania kuna baadhi ya vitu tunavizungumza sana lakini ukienda ngazi za chini havitekelezeki’.



Alisema Watanzania wakiwamo viongozi walianza miaka mingi kuimba wimbo wa ‘Kilimo ni uti wa mgongo’ lakini ukweli ni kwamba hata hao wanaohamasisha wananchi kujikita kwenye kilimo ndani yake hawana hata kitengo cha masoko  na wakiulizwa wanakuwa hawana majibu ya moja kwa moja.



Kongamano hili la siku moja lililoandaliwa na Programu ya kuendeleza mifumo ya kimasoko ya kilimo (AMDT) lilitnguliwa na Mkutano wa siku tatu uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo  Wakulima, wasambazaji wa mbegu, wasindikaji na vyama vya msingi kujadili mnyoro wa thamani kupitia zao la Alizeti.




No comments:

Post a Comment