Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya
uzinduzi kabla ya kuzindua Soko la Madini Chunya.
|
KATIBU Mkuu wa Wizara
ya Madini, Profesa Simon Msanjila amezindua Soko la Madini Chunya ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka Wilaya ya Chunya kuhakikisha
imekamilisha na kuzindua soko la madini ndani ya kipindi cha siku saba. Rais
Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 27 Aprili, 2019 wilayani Chunya katika
mkutano wake na wachimbaji na wachenjuaji wa madini.
Uzinduzi huo
ulishirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa
Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi,
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya
Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo na
Kamishna Msaidizi- Uendelezaji wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Ali Ali.
Wengine walioshiriki
katika uzinduzi huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini
kutoka Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, wawakilishi wa wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi huo, Profesa Msanjila alisema kuwa, tangu kuingia madarakani kwa
Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha
Sekta ya Madini inakua, inanufaisha watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa
Pato la Taifa.
Akielezea mafanikio
ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini, Profesa Msanjila
alisema kuwa, ili kuhakikisha kuwa
wananchi wote wananufahika na rasilimali za madini, Serikali ilitunga Sheria ya
Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa
Maliasili Namba 5 ya Mwaka 2017; Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu
Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Namba 6 ya mwaka 2017 pamoja
na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123.
Aliendelea kueleza
kuwa Serikali pia imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa
wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo na kufafanua kuwa tozo hizo
kuwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio
ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo.
Alisema kuwa, kuwekwa
kwa mazingira mazuri ya kibiashara kwenye sekta ya madini pamoja na kufuta kodi
na tozo mbalimbali zinazofikia asilimia 23 kutaondoa utoroshwaji wa madini na
kusaidia wachimbaji wadogo kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini.
Alieleza manufaa
mengine kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za
wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa mapato ya nchi.
Katika hatua
nyingine, Profesa Msanjila aliwataka
wachimbaji wote wadogo na wafanyabiashara wa madini kuendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na
miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali.
Akielezea manufaa ya
soko jipya la madini Chunya, Profesa Msanjila alisema soko litaziba mianya
ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi na hivyo
kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya
nchi.
Aliongeza kuwa
kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya kutawezesha na kurahisisha biashara nzima
ya madini na kuwa kiungo muhimu cha kuwakutanisha wachimbaji na wafanyabiashara
kwa lengo la kuuza na kununua madini.
Profesa Msanjila
aliendelea kufafanua manufaa mengine ya soko kuwa ni pamoja na kuwa suluhisho
la tatizo la kupunjwa na kudhulumiwa na kuondoa
vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa
vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu kwa baadhi
ya wachimbaji wadogo.
“Soko hili
litaondoa uwezekano wa wanunuzi wa madini kuibiwa na wajanja wachache
wanaojifanya kuwa na madini wakati
hawana, nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko kikamilifu ili kuepuka
udanganyifu na matapeli tu” alisema Profesa Msanjila.
Katika hatua nyingine
Profesa Msanjila aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Chunya, wafanyabiashara wa
madini kwa kuhakikisha Soko la Madini Chunya limezinduliwa ndani ya muda
uliopangwa.
Wakati huo huo
akizungumzia hali ya uanzishwaji wa masoko ya madini nchini, Mwenyekiti wa Tume
ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa, hadi kufikia sasa masoko matano
ya madini yameshafunguliwa katika mikoa ya Geita, Singida, Kahama, Arusha –
Namanga na Chunya.
Aliongeza kuwa masoko mengine ya madini yanatarajiwa
kufunguliwa kabla ya tarehe 05 Mei, 2019 ikiwa ni pamoja na Soko la Madini ya
Dhahabu na Vito vya Thamani Ruvuma, Soko la Madini Shinyanga, Soko la Madini
Dodoma na Soko la Madini Mbeya.
Profesa Kikula alitaja masoko mengine ambayo
yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni kuwa ni pamoja na Soko la Madini ya Bati
(tin) na Soko la Madini ya Dhahabu
Handeni.
Alisisitiza kuwa mikoa mingine ipo katika
hatua za mwisho kukamilisha vigezo mbalimbali vikiwemo vya kiusalama na
miundombinu.
No comments:
Post a Comment