Wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Mnyakongo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma wakifurahia viti na meza walivyokabidhiwa na Benki ya NMB ili kukabili uhaba wa madawati. |
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameiomba Benki ya NMB kutoa elimu kwa wananchi ili wajue jinsi ya kutunza fedha za mikopo yao.
Ndugai ameyasema hayo wakati NMB ilipofanya ziara ya kukabidhi viti na meza 63 vyote kwa Shule ya Mnyakongo pamoja na mabati 250 kwa Shule ya Chiwe zilizopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Spika amesema kuwa NMB inakila sababu ya kuendelea kutoa elimu ya utunzaji fedha kwa wananchi kama wanavyofanya kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ili wawe na ujuzi zaidi. Amesema kuwa wapo watu wengi ambao wanakopa fedha lakini hawajui wafanyie nini baada ya kuzichukua.
"Yaani unashangaa muda mchache ukikutana na watu hao hakuna cha maana walichofanyia badala yake wanarudi katika maisha ya chini badala ya kusonga mbele kimaisha,’’ amesema Ndugai.
Spika Ndugai alisema kutokana na hilo kuna sababu ya elimu hiyo kutolewa kwa wananchi ili wakope fedha huku wakijua wanakwenda kuzifanyia nini. Ndugai amefafanua kuwa ameshakutana na kesi hizo nyingi kwa ndugu jamaa na marafiki ambao wamekopa bila ya kupata mafanikio yoyote.
"Kwa kweli kwa hilo naomba mlifanyie kazi kwani limekuwa likiwaumiza wananchi na kusababisha kurudi nyumba kimaendeleo badala ya kwenda mbele katika maisha kupitia fedha walizokopa,’’ amesisitiza Ndugai.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi amesema kuwa wataendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli hivyo wametenga maeneo manne kwa ajili ya kusaidia jamii.
Mlozi ameyataja amaeneo hayo ni Elimu, Afya, Kilimo na utunzaji fedha kwa vijana mpaka watu wa rika la juu kwa lengo la kuwainua kiuchumi kwa kunufaika kwa kupitia NMB.
Hata hivyo amesema kuwa mpaka sasa tayari milioni 400 zimeshatolewa kwa ajili ya misaada katika shule na hospitli ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa. Mlozi amesema kuwa NMB iko pamoja na serikali kuhakikisha wanafikia malengo waliojiwekea.
Naye Mkuu wa Shule ya Mnyakonga Mpokeeni Sanga amesema kuwa walikua na upungufu wa madawati 70 na wanaishukuru NMB kuwapa viti 63 na meza 63 na ambavyo wanaamini vitasaidia kupunguza uhaba waliokuwa nao.
Sanga amewahakikishia NMB kuwa vitu hivyo watavitunza ili hapo wanafunzi wengine waje kuvitumia hapo mbeleni na amewaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia jamii kwani wamekuwa mfano wa kuigwa nchini.
Mkuu wa Shule ya Chiwe Aron Mango amesema kuwa mabati hayo waliopewa yatawasaidia kuezeka mabweni ya wasichana ambayo yanajengwa shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment