Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Serikali ya Zanzibar Mhe. Balozi Ali Karume akipanda mche wa mti karibu na chanzo cha maji asilia kilichopo Ichenjeziya, Mkoani Songwe. |
WANANCHI waaswa kutunza rasimali mbalimbali katika mazingira yao na kuyapenda ili kuepuka kuathiri na kuharibu mazigira yaliyopo.
Kauli hiyo ameitoa Aprili 1, 2019 mkoani Songwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Ichenjeziya alipotembelea eneo hilo lenye chanzo cha maji ya asili na kupanda mche wa mti ikiwa ni siku ya Kitaifa ya upandaji miti.
Waziri Mhagama alieleza kuwa Nchi yetu imeamua kutumia uchumi wa viwanda ili kutekeleza azma ya Serikali kuelekea uchumi wa pato la kati, hivyo hata upandaji miti na maliasili ya misitu inaendana na uchumi wa viwanda,” alieleza Mhagama.
Aliongeza kuwa kuelekea kwenye Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019, ni vyema wananchi wakashiriki kauli mbiu ya upandaji miti ambayo inaendana na kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
“Wanaichenjeziya mnatakiwa kuweka historia kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu kwa kupanda miti kwenye vyanzo vya Maji ili kupata maji safi na salama,” alisema Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa kila mwananchi kuhakikisha anakuwa msimamzi wa mazingira na anatunza vyanzo vya maji kwa kufuata sheria na taratibu ili kuhakikisha kila mtu anafikiwa na maji safi na salama kama haki ya msingi.
Hata hivyo Mhe. Mhagama alitumia pia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wa Songwe na Mikoa ya jirani kushiriki kwa wingi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazozinduliwa Aprili 2, 2019 katika Uwanja wa Kimondo uliopo Kata ya Forest, Wilayani Mbozi.
“Hii ni nafasi ya kipekee kwa wananchi na ni siku ya kuhamasishana kwa vijana kwa kujitathimini na kutambua mchango wa Baba wa Taifa na Mhasisi wa Mapinduzi ya Zanzibari katika kujenga Taifa,” alisema mhagama
Naye Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Ali Karume alisema kuwa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ni siku muhimu sana kwa wananchi kutambua historia ya Tanzania Bara na Zanzibar iliyopelekea Taifa katika mwanga.
No comments:
Post a Comment