SERIKALI KUFUNGA RADA NYINGINE MBILI ZA HALI YA HEWA MKOA WA MBEYA NA KIGOMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 1 April 2019

SERIKALI KUFUNGA RADA NYINGINE MBILI ZA HALI YA HEWA MKOA WA MBEYA NA KIGOMA

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi (kushoto) akisaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za mamlaka hiyo na mwakilishi wa Kampuni ya Enterprise Electronics Corporation (ECC), Edwin Kasanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Infratech Ltd (T) leo jijini Dar es Salaam. Tukio hilo limeshuhudiwa na Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye (katikati waliosimama) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dk. Buruhani Nyenzi (kushoto nyuma).


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi (kushoto) akisaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za mamlaka hiyo na mwakilishi wa Kampuni ya Enterprise Electronics Corporation (ECC), Edwin Kasanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Infratech Ltd (T) leo jijini Dar es Salaam. Tukio hilo limeshuhudiwa na Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye (wapili kulia waliosimama) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dk. Buruhani Nyenzi (wa pili kushoto nyuma). Wengine ni wanasheria wa pande zote, Emmanuel Ntenga wa TMA (kushoto) na Queen Allen wa ECC.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi (kushoto) wakibadilishana nakala za mkataba huo na Mwakilishi wa Kampuni ya Enterprise Electronics Corporation (ECC), Edwin Kasanga ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Infratech Ltd (T) leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutiliana saini. Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi (kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Kampuni ya Enterprise Electronics Corporation (ECC), Edwin Kasanga (kulia)  wakionesha nakala za mikataba leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutiliana saini ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Kawetere katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na eneo la Nyamoli katika barabara ya kuelekea Bulombora, Kigoma na hivyo kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya mtandao wa rada tano (5).

Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye (katikati) akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Kawetere katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na eneo la Nyamoli katika barabara ya kuelekea Bulombora, Kigoma na hivyo kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya mtandao wa rada tano (5). 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi akijibu maswali ya wanahabari mara baada ya kusaini mkataba huo. Kulia ni Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye.

 
SERIKALI ya awamu ya tano imejizatiti katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinakuwa za viwango vya kimataifa na za usahihi wa hali ya juu. Katika kufanikisha hili Serikali ya awamu ya tano iliahidi kuendelea kuongeza mtandao wa Rada za hali ya hewa ili kufikia Rada saba (7) zinazohitajika kwa nchi nzima.

Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, imesaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Kawetere katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na eneo la Nyamoli katika barabara ya kuelekea Bulombora, Kigoma na hivyo kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya mtandao wa rada tano (5).

Ikumbukwe kuwa tayari Mamlaka imeishafunga rada mbili za hali ya hewa huko Kiseke Mwanza na Bangulo Dar es Salaam pia imeanza utaratibu wa ufungaji wa Rada Mtwara. Hii inaifanya Tanzania kuwa Taasisi bora kwa uangazi wa wa hali ya hewa kwa njia ya Rada katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ununuzi wa Rada hizi mbili (ya nne na ya tano) kwa ajili ya Mbeya na Kigoma umegharimu kiasi cha Tshs. 5,715,971,148.45 (USD 2,497,125) kwa kila moja na pia utengenezaji na ufungaji wa rada zote mbili utachukua muda wa miezi kumi na nne hadi kukamilika kwake.  Mtengenezaji wa Rada hizo ni Enterprise Electronics Corporation (ECC).

Rada hizi zina uwezo wa kuona hadi kilometa za mkato 450 (Aerial distance) huku zikizunguka (radius distance) na uwezo halisia wa kuona mpaka matone madogo sana ya mvua ni kilometa za mkato 250.

Rada za hali ya hewa ni moja ya mitambo inayotumika kufanya uangazi wa hali ya hewa wa masafa marefu. Mitambo hii husaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisia wa anga kipindi Radar inapozunguka. Rada inasaidia;
·         Kujua kwa wakati maeneo yenye mvua, aina ya mawingu yaliyopo na wakati mwingine hata kujua ni kiasi gani cha mvua kinachotarajiwa.
  • Kufuatilia maeneo yenye mvua kubwa na za mawe zinazoambatana na radi na upepo mkali hivyo kuweza kutoa tahadhari kwa muda muafaka.

  • Kufuatilia muelekeo wa mifumo inayosababisha hali mbaya ya hewa (mvua za mawe, upepo mkali na dhoruba).

  • kufuatilia vimbunga baharini kadri ya upeo wake na hivyo kuweza kutoa tahadhari kutokana na mwenendo wa vimbunga hivyo.

  • Kufuatilia upepo unaoweza kuleta madhara kwa usalama wa usafiri wa anga (wind shear) na


  • Kutoa ushauri kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa ili wachukue tahadhari wakati wa shughuli zao kiuchumi na kijamii.

  • Kusaidia kutoa utabiri wa muda mfupi na wakati wa hali mbaya ya hewa.

Kwa kumalizia napenda kuwashukuru kwa ushirikiano wenu katika kusambaza taarifa za hali ya hewa na napenda kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika kulinda na kutunza mitambo hii ya Rada pamoja na vifaa vyote vya hali ya hewa kwa manufaa ya Taifa letu.
Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)



No comments:

Post a Comment