Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua
Mkutano Mkuu wa Sita wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri
(REDOA) kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Machi 26, 2019. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mwenyekiti wa
Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri (REDOA), German Mung'aho
baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Sita wa REDOA kwenye ukumbi wa Chuo cha
Mipango jijini Dodoma, Machi 26, 2019. Wa pili kulia ni Waziri wa
Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, kushoto ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma, Patrobas Katambi. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa
na Wilaya wanaoshirikiana na waliamu kujihusisha na wizi, udanganyifu na
uvujaji wa mitihani waache mara moja tabia hiyo na mwenendo huo kwa sababu
unalivunjia heshima na hadhi Taifa.
“Kamati
za Mitihani za Mikoa na Wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu
bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi
kwa mujibu wa sheria.Hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika
kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”.
Waziri
Mkuuametoa onyo hilo leo (Jumanne, Machi 26, 2019) wakati wa ufunguzi wa
Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya(REDEOA),
uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Kauli mbiu ya
mkutano huo inasema “Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo
2025”
AmesemaBaraza
la Mitihani la Tanzania (NECTA) ni chombo ambacho kwa muda mrefu kimejijengea
sifa kubwa sana nchini na barani Afrika, ambapo Serikali imewekeza kiasi
kikubwa cha rasilimali ili kukifanya chombo hiko kuwa imara na cha
kisasa.
Waziri
Mkuu amesema hali hiyo imezifanya nchi mbalimbali kuja nchini kujifunza masuala
ya upimaji na uendeshaji wa mitihani. “Nimejulilishwa pia hivi sasa hapa nchini
wapo Viongozi wa Mabaraza ya mitihani kutoka nchi za Afrika Mashariki”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema suala la tatizo la
nidhamu mbaya ya wanafunzi ni jukumu la walimu wote, hivyo wanatakiwa
watekeleze majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na kuwaendeleza
wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kuzingatia sheria.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imesikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya athari
ya viboko kwa wanafunzi shuleni ikiwemo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu
pamoja na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa shule ya msingi
Kibeta Mkoani Kagera.
“Ninatambua
si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu
katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni. Maafisa
Elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa adhabu
shuleni chini ya kifungu cha 61 cha sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni
zake”.
“Adhabu
ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa
litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Na
adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina
hakika tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma”.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya
hao kwa sababu wanafanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu wa
kidato cha sita na cha nne nchini. Amewasisitiza waendelee kufanya kazi kwa
bidii.
Naye, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka maafisa hao
wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Awali,
Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema umoja wao unatekeleza majukumu
yao ya kusimamia elimu kikamilifu nchini, lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais
Dkt. John Magufuli, ambaye anasisitiza watu wafanye kazi.
Amesema umoja huo una wanachama
zaidi ya 400 na ulianzishwa ili kusimamia utoaji wa elimu nchini. Katika
mkutano huo wanatarajia kujadiliana changamoto mbalimbali za sera ya elimu na
namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo
ameiomba Serikali iwapatie magari maafisa hao watakayoyatumia kwa ajili ya
kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao ya kazi, ambapo Waziri Mkuu
amesema suala hilo linashughulikiwa.
No comments:
Post a Comment