TMA YATABIRI MVUA KUBWA MIKOA YA IRINGA, NJOMBE, MBEYA, SONGWE, RUKWA NA MOROGORO...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 30 March 2019

TMA YATABIRI MVUA KUBWA MIKOA YA IRINGA, NJOMBE, MBEYA, SONGWE, RUKWA NA MOROGORO...!

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi akizungumza. (Picha na maktaba yetu).

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo katika utabiri wake wa mwelekeo wa hali ya hewa wa muda mfupi na muda wa kati, huku ukionesha uwepo wa mvua kubwa  mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Morogoro (Mahenge).

Taarifa hiyo pia imeitaja mikoa mingine ya Lindi na Mtwara kutarajia mvua hizo ambazo zitaanza kujitokeza katika kipindi cha mwisho wa wiki kuanzia tarehe 30 Machi hadi 3 Aprili, 2019.

Katika taarifa hiyo ya TMA imebainisha kuwa mwenendo wa mvua kipindi hiki hautarajiwi kubadili matarajio ya jumla ya mvua za Masika, hivyo msimu unatarajiwa kuwa mfupi na vipindi vya upungufu wa mvua za masika vikijitokeza maeneo mengi.

Imeeleza mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi yanayopata mvua za masika baada ya athari ya upungufu wa mvua uliotokana na vimbunga vilivyojitokeza mfululizo katika bahari ya Hindi ikiwemo kimbunga Idai, Savannah na Joaninha katika mifumo ya hali ya hewa kuanza kupungua.

Hata hivyo vipindi vya mvua vinatarajiwa kuongezeka katika baadhi ya maeneo katika wiki mbili zijazo za mwezi Aprili, 2019. Maeneo ya mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Kilimanjaro ambayo yalikumbwa na upungufu wa mvua kutokana na vimbunga hivyo. Huku hali hiyo ikitarajiwa kuanza kupata mvua katika kipindi hiki cha mwishoni mwa mwezi Machi na wiki ya kwanza ya mwezi Aprili, 2019.

Pamoja na hayo, ongezeko la mvua linatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara hususan katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019 kwa siku chache.

"...Mwanzoni mwa mwezi Aprili, 2019 vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika mkoa wa Morogoro na kusambaa katika maeneo machache ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam." Imesema taarifa hiyo ya TMA.

TMA imeshauri Wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri za mamlaka na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment