MAFUNZO YA TATHIMINI YA VIMELEA HATARISHI VYA MAGONJWA KWA DHANA YA AFYA MOJA YAFANYIKA KWA MARA YA KWANZA BARANI AFRIKA NCHINI TANZANIA. - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 31 March 2019

MAFUNZO YA TATHIMINI YA VIMELEA HATARISHI VYA MAGONJWA KWA DHANA YA AFYA MOJA YAFANYIKA KWA MARA YA KWANZA BARANI AFRIKA NCHINI TANZANIA.


Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akifafanua umuhimu wa Tathmini  ya vimelea hatarishi vya magonjwa kwa kutumia Dhana ya Afya moja wakati  wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta za afya nchini , Jijini Dar es salaam.


Baadhi ya wawezeshaji wa hapa nchini Tanzania na wamashirika ya Kimataifa  wakiendesha mafunzo ya Tathmini  ya vimelea hatarishi vya magonjwa kwa kutumia Dhana ya Afya moja wakati  wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta za afya nchini, Jijini. 
KWA mara ya kwanza Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kufanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Afya moja juu ya namna ya  kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya magonjwa kwa kutumia dhana ya Afya moja. Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalam na wadau wa Afya moja kutoka sekta mbalimbali, hususan sekta za afya ya binadamu, wanyama, kilimo na mazingira.

 
Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua katika uratibu wa  masuala  ya Afya moja, ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na  mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu, hali hiyo imechagiza kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa wataalam wa sekta za  Afya hapa nchini kupewa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 25-28 Machi, 2019, Jijini Dar es salaam, yaliendeshwa na wataalamu kutoka Makao makuu ya  Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya Shirika la Chakula Duniani (FAO), pamoja na Shirika linaloshughuliks na Afya ya Wanyama (IOE). Wataalamu hao wameweza kuwapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya hapa nchini juu ya namna ya kufanya tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha mbwa, Kimeta na Homa ya Mafua ya ndege.

Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, alibainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na sekta za Afya  kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua kuwa  dhana hiyo inapunguza gharama katika kushughulikia tishio la magonjwa  yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa vimelea vya magonjwa.
 
Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo  hayo wamebainisha kuwa  wamekuwa wakifanya tathmini za vimelela hatarishi vya magonjwa hapa nchini lakini tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta kwani hazikuwa zinazingatia ushirikiano kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha walifafanua kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuandaa nyenzo ya kitaifa ya kufanya Tathimini kwa Dhana ya Afya Moja ambayo itawaongoza Wataalamu  hususani wanapokuwa katika maeneo halisi yanakotokea magonjwa.

Aidha, washiriki  hao walieleza kuwa Dhana ya Afya Moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea vingi vinavyo sabababisha magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka  kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi yanatokea pale binadamu anapoingilia maskani ya wanyama hao bila tahadhari. Hata hivyo, kwa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuzingatia kuwa Bara la Afrika hususan sehemu zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama (Congo Basin) ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa(RVF), Marburg na mengineyo.

Walibainisha kuwa, Kupitia matokeo ya mwingiliano kati ya wanyama na binadamu, wadau wa afya moja wanawajibika kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia, kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha  wataalam wa sekta mbalimbali za  afya jinsi ya kufanya tathmini ya  hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano. 

Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo  Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja  kwa kushirikiana na WHO, FAO, IOE na wadau wengine wa Afya moja waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.

No comments:

Post a Comment