WAMILIKI WA LESENI ZA UCHIMBAJI MADINI ZISIZOTUMIKA MKOANI MOROGORO WAKALIA KUTI KAVU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 27 February 2019

WAMILIKI WA LESENI ZA UCHIMBAJI MADINI ZISIZOTUMIKA MKOANI MOROGORO WAKALIA KUTI KAVU

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akitoa maelekezo kwa wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kupata idadi ya nyumba zinazotakiwa kulipiwa kodi ya Majengo, wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri huyo na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na watumishi wa TRA, Mkoani Morogoro, kushoto ni Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro Bw. Emmanuel Maro.

Na Peter Haule, Morogoro
SERIKALI imeahidi kulifanyiakazi suala la Leseni mfu za uchimbaji madini mkoani Morogoro, ili kutoa fursa ya wachimbaji wadogo  kuchimba madini hayo na kulipa kodi stahiki kwa manufaa mapana ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipofanya Mkutano na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoani Morogoro na wadau wengine.
Maelekezo hayo yanafuatia maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe, ambaye pamoja na kuishukuru Serikali kwa  kutoa fedha zenye lengo la kuzisaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato na akaiomba Serikali kuhakikisha inafuta Leseni mfu za wachimba madini takribani 174 ambao wanazuia wachimbaji wadogo kufanya shughuli za kujipatia kipato kutokana na  madini na kulipa kodi.
Dkt. Kabwe alimweleza Dkt. Kijaji kwamba mkoa wa Morogoro umesheheni madini ya kila aina na jambo linalosababisha ukosefu wa mapato unachangiwa pia na  utoroshaji wa madini ambapo ameeleza kuwa mikakati ya Mkoa huo ni kuanzisha Soko la Madini mkoani humo ili kuepusha utoroshaji huo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa kama wapo watu wenye Leseni za uchimbaji madini 178 na wanaolipa kodi ni wanne pekee hakukuwa na sababu ya kuendelea kuwa nao, hivyo atalifikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamana ya madini ili kuangalia ni namna gani wachimbaji wadogo wataweza kupewa fursa hiyo ili waweze kujipatia kipato na kulipa kodi.
Akizungumza kuhusu uwezo wa nchi kujitegemea kimapato, Dkt. Kijaji alisema kuwa Tanzania imepunguza utegemezi na kufikia asilimia 12, na kwamba  fursa nyingi za kimapato hazijatumika kikamilifu na kutoa wito kwa kila kiongozi na watumishi kuwajibika kikamilifu katika maeneo yao ya kazi ili Taifa liweze kujitegemea zaidi.
 “Wanafalsafa mbalimbali wanasema Taifa lisilojitegemea kimapato ni watumwa, Taifa lisilojisimamia kwa mapato yake halijapata uhuru kamili kwa sababu mapato ndio moyo wa Taifa lolote na  mapato ya Taifa lolote ndio usalama wa Taifa hilo”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema Taifa likiwa imara kimapato hakuna yeyote atakae lichezea hasa likiwa limejiimarisha kwa mapato ya ndani,  kwa kuwa  mapato yanasababisha kuwa na uhuru wa kufikiri na kupanga mipango ya maendeleo bila kusubiri kupangiwa na watu wengine.
Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa ni lazima kuhakikisha  mianya yote ya ukwepaji kodi inafungwa na  kuzuia matumizi yote yasiyo ya lazima ili kuzielekeza fedha hizo kwenye maeneo yenye maslahi mapana ya Taifa.
Alisema kodi zinazokusanywa, matokeo yake yanaonekana ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo umefikia asilimia 42 katika utekelezaji wake.
Aidha vijiji zaidi ya 3,500 vimewashwa umeme ndani ya miaka miwili ya uongozi wa awamu ya Tano, Hospitali 67 kwenye halmashauri nchini zimeanza kujengwa na  Tanzania inaangaza Dunia baada ya kununua ndege zake kwa  mapato ya ndani kutokana na  kuiishi falsafa ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Amewataka viongozi wa Mkoa huo na watumishi wengine kuhakikisha wanatenda kile walichoamriwa katika nafasi zao kwa bidii na kuepukana na rushwa kwa kuwa Taifa litajengwa na wazalendo  na sio wenye meno.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo Bi. Siriel Mchembe alieleza kuwa  ni vema kuwa na uhusiano mzuri kati ya Uongozi wa Mkoa, Wilaya na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na uongozi wa vijiji na mitaa ili kuwa na kanzi data hasa ya majengo ili kuhakikisha makusanyo yanaongezeka na lengo la Mkoa kukusanya Sh.  Bilioni 91 kwa mwaka linafikiwa.
Dkt. Kijaji anaendelea na ziara ya kukagua miradi iliyopewa fedha na Serikali ikiwemo ya Kimkakati Mkoani Morogoro iliyo na lengo za kuzisaidia Halmashauri kujitegemea kimapato

No comments:

Post a Comment