Picha ya pamoja ya viongozi waandamizi wa kampuni zote mara baada ya hafla ya kusaini mkataba huo wa ushirikiano kibiashara. |
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation, kupitia
mtandao wake wa huduma za kifedha wa T-PESA pamoja na wadau wa kibiashara,
Kampuni tatu kutoka nchini Korea zimesaini mradi wa kutengeneza mfumo wa malipo
kwa kutumia kadi (T Card).
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya
TTCL leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Huduma za T- PESA Ndugu Moses Alponce,
alisema mfumo huo unaotumia teknolojia za kisasa ni matokeo ya utafiti
uliofanywa na kuonesha mahitaji makubwa ya huduma za malipo yasiyotumia fedha
tasilimu.
Aidha aliongeza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutarahisisha
shughuli za kibiashara na kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
katika kukusanya kikamilifu kodi za Serikali kutoka kila miamala
itakayofanyika, sambamba na kuongeza ufanisi katika biashara na shughuli
nyingine za kiuchumi.
Mfumo huo unaotekelezwa na T-Pesa kwa kushirikiana na wadau
wake kibiashara kutoka Jamhuri ya watu wa Korea katika muunganiko wa Kampuni
tatu, ambazo ni PayLink Korea, KEH Hana Card pamoja na ATECT & Company
unakuwa wa kwanza kuletwa na huduma za fedha kwa kutumia simu za mikononi
nchini Tanzania.
"..Kampuni hizi zitashirikiana na T PESA katika zoezi
la kuandaa, kupanga na kutengeneza Mfumo wa kadi za NFC na POS Cashless
Ecosystem," alisema Alponce.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya PayLink ya Korea,
MoonKyu Lee akiwakilisha kampuni hizo alisema kuingia kwa ushirikiano katika
mfumo huo utaongeza uwazi katika miamala ya kifedha jambo ambalo litaongeza
mapato ya kodi kwenye mifumo ya malipo nchini na kuleta maendeleo.
Ikiwa sasa ni takribani miaka miwili tangu kuanzishwa kwake,
T PESA imekuwa na mchango mkubwa katika huduma za Fedha mtandao Nchini, ambapo
kwa mujibu wa ripoti ya TCRA toleo la mwaka 2019, T PESA ni moja ya huduma zinazokua
kwa kasi kubwa ikiwa na Mawakala 10,000, wateja laki 320,000 wanaozungusha
miamala ya takribani Tsh Bilioni 4.
No comments:
Post a Comment