Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa Afisa
Usalama Msaidizi wa Uwanja wa Ndege wa Katavi, Fredrick Valentine(wa kwanza
kulia) wakati akikagua miundombinu na hali ya uwanja huo akiwa ziarani mkoani
humo. Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi (wa tatu kulia) akifuatilia kwa
makini mazungumzo hayo.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akikabidhi
kompyuta kwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi (wa pili kulia) kwa ajili
ya shule za sekondari mjini humo. Wakishuhudia, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi
wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Albert Richard na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abdallah Malela (wa pili kushoto).
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa
viongozi wa Mkoa wa Katavi, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na waalimu wa
sekondari (hawapo pichani) kuhusu ukuaji na maendeleo wa sekta ya Mawasiliano
nchini. Kulia kwake ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Mhe. Sebastian Kapufi na kushoto
ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Abdallah Malela.
Mkurugenzi wa
Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Albert Richard akitoa
maelezo ya kompyuta walizotoa kwa shule za sekondari za Mpanda. Walioketi
wakimsikiliza, wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Atashasta Nditiye na katikati ni
Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi.
NAIBU Waziri wa Uchukuzi
na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amekabidhi kompyuta 25 kwa shule za
sekondari Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kukuza kiwango cha ufaulu na
kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) shuleni kwa
kuwawezesha waalimu kutumia kufundishia na wanafunzi kujifunzia.
Nditiye amewataka
waalimu na wanafunzi wa shule hizo kuhakikisha kuwa kompyuta zilizotolewa
zinatumika kwa nia njema kutoa elimu kwa watoto wetu kwa kuwa sasa dunia ni
kijiji. Amefafanua kuwa lengo ni tupate wanafunzi mahiri kwa kompyuta hizo
kutumika na wanafunzi wengine kwenye shule mbali mbali kwa kuziunganisha
kompyuta hizo kwenye mtandao ili mwalimu mmoja aweze kufundisha wanafunzi wengi
wengine wa shule nyingine
“Kumbukeni hapo zamani
wanafunzi wa mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma ilikuwa inatoa wanafunzi wenye
ufaulu mzuri, hivyo tuwarithishe wanafunzi wetu,” amesisitiza Nditiye.
Kompyuta hizo
zimetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao una dhamana ya kuhakikisha wananchi waishio
vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wana wasiliana kwa kuzipatia
kampuni za simu za mkononi ruzuku ya kujenga minara ili kufikisha huduma za
mawasiliano maeneo mbali mbali nchini.
Nditiye amekabidhi
kompyuta 25 zenye thamani ya shilingi milioni 46 kwa Mbunge wa Mpanda Mjini,
Mhe. Sebastian Kapufi kwa niaba ya waalimu na wanafunzi wa shule za sekondari
zilizopo mjini humo kwa kuwa aliiomba Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na
nusu ili shule hizo ziweze kupatiwa
kompyuta hizo.
“Nimeanza kumsumbua
Nditiye zaidi ya mwaka mmoja na nusu kuomba kompyuta, unaweza kuona kompyuta ni
chombo chepesi ila sio hivyo kwa kuwa ni chombo muhimu na kitatunza siri,”
amesema Kapufi.
Pia, ameongeza kuwa
tunalotekeleza hapa ni upendo na na litaenda kufuta ujinga wa watoto wetu
kwenye shule za sekondari kwa kutumia kompyuta hizi. Vile vile ameishukuru
Serikali kwa ahadi ya mafunzo ya kompyuta ambayo yatatolewa kwa waalimu wa
shule ili kuwawezesha namna ya kutumia na kufanyia matengenezo madogo madogo
kompyuta hizo ambapo ameahidi kuwa atakwenda yeye mwenyewe binafsi kukabidhi
kompyuta hizo kwa kila shule.
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka UCSAF
Mhandisi Albert Richard amesema kuwa UCSAF imekuwa ikitoa kompyuta hizo kwenye
shule mbali mbali nchini kupitia mradi wa kuunganisha shule ujulikanao kama
“School Connectivity”. Richard amesema kuwa ni imani yao kuwa kompyuta hizo
zitatumika kwa malengo yaliyopangwa kwa nia ya kuwasaidia wanafunzi kusoma na
waalimu kufundishia. Ameongeza kuwa UCSAF itatoa mafunzo kwa waalimu wa shule
za sekondari za Mpanda ya namna ya kutumia kompyuta hizo kufundushia pamoja na
waalimu wao wenyewe kuweza kuzifanyia matengenezo madogo madogo kompyuta hizo
pale zinapoharibika.
Akizungumza kwa niaba
ya waalimu wa shule za sekondari za Mpanda, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa
ya Mpanda, Enelia Lutungulu amesema kuwa shule za msingi na sekondari zina
uhitaji mkubwa sana wa kompyuta kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia
na TEHAMA ambapo kazi nyingi zinahitaji mawasiliano kwa kutumia kompyuta
“Shule hizi zina
uhitaji mkubwa wa kompyuta kwa kuwa baadhi ya shule kompyuta zinazotumika ni za
waalimu binafsi na hivyo kuleta ugumu wa utendaji wa kazi wa kila siku
ukizingatia upokeaji na utoaji wa taarifa ni wa kila mara,” amefafanua
Lutungulu.
Ameongeza kuwa
kompyuta hizo zitakuwa kichocheo cha kuongeza na kurahisisha ufanisi wa kazi
katika shughuli mbali mbali zikiwemo za uchapishaji wa mitihani ndani ya shule,
ukusanyaji na uhifadhi wa data za kielimu katika shule, utoaji rahisi na wa
haraka wa taarifa kwa kutumia TEHAMA, kupokea miongozo na maagizo mbali mbali
ya kikazi kwa kutumia mawasiliano ya barua pepe, kwenda sambamba na mabadiliko
ya sayansi na teknolojia ikiwemo TEHAMA na mawasiliano katika kazi za kila
siku. Makabidhiano ya kompyuta hizo yamehudhuriwa na wakuu wa shule za
sekondari, viongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Wilaya
ya Mpanda na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya hiyo.
Akiwasilisha taarifa
ya mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Abdallah Malela amemuomba Nditiye kuipatia
mkoa huo ofisi ya TTCL ya ngazi ya mkoa tofauti na hali ilivyo sasa ambapo ipo
ofisi ya TTCL ya ngazi ya wilaya. Pia, ameongeza kuwa mkoa upatiwe usafiri wa
ndege kwa kuwa ina kiwanja kizuri na kuna wateja wa kutosha.
Nditiye amepokea
changamoto hizo na kuielekeza Bodi ya TTCL na menejimenti yake kufungua ofisi
ya Shirika hilo lenye hadhi ya mkoa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Pia,
ameuhakikishia uongozi wa mkoa na wananchi wa Katavi kuwa Serikali inaleta gari
la zimamoto kwenye uwanja huo na huduma za usafirishaji utaanza kutolewa kwa
wananchi na wadau wa mkoa huo. Pia, Nditiye alitembelea na kukagua kiwanja
hicho cha ndege na kuona hali ya kiwanja na miundombinu yake.
No comments:
Post a Comment