DK MPANGO AZIONYA TAASISI ZA SERIKALI ZISIZOTUMIA MFUMO WA KIELETRONIKI KUKUSANYA MAPATO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 24 February 2019

DK MPANGO AZIONYA TAASISI ZA SERIKALI ZISIZOTUMIA MFUMO WA KIELETRONIKI KUKUSANYA MAPATO

Waziri wa Fedha na Mipango  Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango  akisalimiana na Wenyeviti wa Taasisi Binafsi waliohudhuria mkutano uliowakutanisha Mawaziri mbalimbali, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Wafanyabiashara uliolenga kukuza biashara mkoani humo, kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC mkoani Arusha.

Na Josephine Majura na Ramadhani Kissimba,  Arusha

WAZIRI wa Fedha  na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amezitaka Taasisi zote za Serikali kutumia kikamilifu mfumo wa malipo wa Serikali wa kielektroniki (GePG), ili kutimiza azma ya Serikali ya kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za Umma.

Dkt. Mpango ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha wafanyabiashara wa sekta ya madini, utalii, mahotel na viwanda wa Mkoa wa Arusha kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Akijibu hoja na kutolea ufafanunuzi wa kero mbalimbali zilizowasilishwa na Wafanyabiashara hao, Dkt. Mpango alisema Serikali ilishatoa maagizo kwa Taasisi zote za Serikali kuwa malipo yote yafanyike kwa kutumia mfumo wa malipo ya Serikali, na endapo itatokea Taasisi yoyote itashindwa kufanya hivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Serikali iliziagiza Taasisi zote kuanza kutumia mfumo wa malipo ya Serikali ifikapo mwezi Juni, 2019, na nina agiza kuanzia leo mwananchi yeyote asikubali kulipa malipo yoyote yasiyotumia mfumo huu” alisisitiza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia  Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini.

Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo, kwa lengo la kutatua kero mbalimbali za Wafanyabiashara wa Mkoa huo, na kuhudhuriwa na  Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais Mazingira Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Isack Kamwele,  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu, na Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde.

No comments:

Post a Comment