WAZIRI HASUNGA AMFANANISHA RAIS MAGUFULI NA NYERERE KWA MATENDO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 28 December 2018

WAZIRI HASUNGA AMFANANISHA RAIS MAGUFULI NA NYERERE KWA MATENDO

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akiwa amesimama kwenye msingi wa jengo la Wizara ya Kilimo katika eneo la Ihuma pembeni yake kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na wengine ni Msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo kutoka SUMA JKT  Mhandisi Meja Onesmo Njau.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na Fundi Mkuu wa ujenzi wa jengo hilo kutoka SUMA JKT  Mhandisi Meja Onesmo Njau baada ya kuonyeshwa ramani ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Kilimo katika eneo la Ihumwa leo baada ya kutembelea eneo hilo.

WAZIRI wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema namna ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Joseph Magufuli anavyoongea na kutenda ni sawa  Mwasisi wa  Taifa la Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mhe. Hasunga ameyasema hayo leo alipotembelea eneo la Ihumwa ambapo ujenzi wa ofisi mpya za Wizara ya Kilimo zimeanzwa, Jijini Dodoma.

Mhe. Hasunga amesema Baba wa Taifa Mwalimu Kambarage Nyerere ndiye aliyetoa wazo la Dodoma kuwa makao ya Chama Tawala pamoja na Serikali lakini kwa miaka kadhaa wazo hilo lilikuwa halijawahi kutekelezwa na kuongeza kuwa Rais Magufuli ndiye amelitekeleza kwa vitendo.

Waziri wa Kilimo ameongeza kuwa baada ya utekelezaji wa wazo hilo la kuhamia Dodoma kwa Serikali, Rais Magufuli aliagiza Wizara zote zijenge ofisi katika eneo moja na kwa kulitekeleza jambo hilo, Wizara zilipewa mgao maalum wa fedha kwa ajili ya kujenga ofisi za kudumu katika eneo la Ihumwa.

“Napenda nimpongeze Mhe. Rais wetu kwa kulisimamia wazo hili la kuwa na eneo maalum na rasmi la kuwa ofisi kwa Wizara zote na moja kati ya faida ni kuwa Wananchi ambao wamekuwa wakisafiri kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupata huduma katika ofisi za umma, sasa watapata unafuu wa kuhudumiwa katika eneo moja kama hapa, ambapo kila Wizara itapatikana.” Amekaririwa Mhe. Hasunga.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa, jambo hili ni sawa na utekelezaji wa Oparesheni Sogeza ambapo, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alianzisha katika mwaka 1974 lengo likiwa ni kuhakikisha Wananchi wanakaa pamoja ili Serikali iwahudumie kwa haraka zaidi na kwa ufanisi zaidi.

“Wazo la Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuhamia Dodoma na Ofisi za Serikali kukaa pamoja hivi, jambo hili linafanana na wazo la Baba wa Taifa kupitia Oparesheni Sogeza ambapo Wananchi wanawekwa pamoja ili Serikali iwajibike sawasawa kwa Wananchi”. Amekaririwa Mhe. Hasunga.

Mhe. Hasunga amefanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Kilimo ambapo kwa kuanzia Wizara inajenga ofisi za Wakuu wa Idara na Vitengo na baadae zitajengwa ofisi wa Watumishi wengine wa Wizara katika eneo hilo la pamoja.

Akizungumza kuhusu kukamilika kwa ujenzi huo, Waziri Hasunga amesema Mkandalasi alipewa lengo la kukamilisha ujenzi huo tarehe 31/12/2018 lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, kazi hiyo inataraji kukamilika tarehe 12 Februari, 2019.

Naye Fundi Mkuu wa majengo ya Wizara ya Kilimo, Mhandisi Meja Onesmo Njau amesema kama ambavyo Mpango kazi wao unavyooshesha kazi kuanza rasmi tarehe 10 Disemba, 2018 na kwamba wanataraji kukamilisha na kukabidhi rasmi tarehe 12 Februari, 2019 na kuongeza kuwa Tasisi yao ya SUMA JKT imepewa jukumu muhim na la heshima na kwamba watamaliza kwa wakati.

No comments:

Post a Comment