NA LUSUNGU HELELA, MWANZA
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Halmashauri ya wilaya Buchosa mkoani Mwanza kupitia upya ramani ya vijiji vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Kisiwa cha Maisome kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wanavijiji na Halmashauri hiyo.
Ameuagiza Uongozi wa Halmashauri hiyo ushirikiane na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakati wa inapofanya upya mapitio ya ramani hiyo ili kuweza kumaliza tatizo la mgogoro huo uliopo kufuatia baadhi ya maeneo ya wananchi kuingia ndani ya Hifadhi ya msitu huo kwa mujibu ramani iliyopo.
Ametoa agizo alipokuwa wilayani humo kwa ziara ya siku mbili ya kutatua kero za wananchi mara baada ya kusikiliza malalamiko kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Kisaba na Busikimbi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanya katika kijiji cha Kisaba wakidai kuwa TFS imechukua baadhi ya maeneo ya vijiji hivyo.
Katika vijiji hivyo jumla ya ekari 103 za wananchi walizokuwa wakizitumi katika shughuli za kiuchumi zinadaiwa kuingia ndani ya Hifadhi ya msitu iliyo chini ya TFS.
Naibu Waziri Kanyasu amefafanua kuwa hakuna mgogoro kati ya TFS na wananchi ila kuna mgogoro kati ya wananchi na Halmashauri waliotengeneza ramani hiyo na sio TFS.
Daniel Serengeti ni mkazi wa kijiji cha kisaba ambaye shamba lake limemegwa ameiomba serikali kuwarudishia maeneo hayo kwa kuwa walikuwa wanayamiliki tangu mwaka 1968.
"wachora ramani sio TFS, Hivyo TFS wanatumia ramani iliyokwisha tengenezwa na Halmashauri hiyo kutokana na hilo wanatakiwa kupitia upya na kuondoa mgogoro", alisema Kanyasu.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Buchosa Crispin Luanda amesema kuwa maagizo hayo atayatekeleza kwa wakati ili kufanikisha swala hilo .
Amesema mara baada ya ramani mpya itakapokamilika itapelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya urekebishaji wa maeneo hayo.
Katika hatua nyingine, Kanyasu ameruhusu upanuzi wa njia itakayopita ndani ya Hifadhi ya Maisome kwa ajili ya kuwapunguzia adha wakazi walio wengi wanaokwenda katika Kambi ya Uvuvi ya Bugombe kwa ajili ya kujipatia mahitaji muhimu ya kila siku.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Dk. Charles Tizeba amemshuru naibu wa Waziri huyo kwa kutatua mgogoro huo ambao ulikuwa kero kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment