WAZIRI KAMWELE AWATAKA TANROADS KUFANYAKAZI KWA KUSHIRIKIANA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 10 November 2018

WAZIRI KAMWELE AWATAKA TANROADS KUFANYAKAZI KWA KUSHIRIKIANA


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe, Eng.  Isack Kamwelwe akikabidhi moja ya kitendea kazi kwa Mwenyekiti wa Bodi mpya ya TANROADS Dakta, Damas Lucas Nyahoro katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya TANROADS na kuiaga Bodi inayomaliza muda wake mjini Dodoma.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amezungumzia umuhimu wa kushirikiana baina ya Bodi,Menejimenti na Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), ili kufikia malengo kwa wakati.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua Bodi mpya ya TANROADS na kuiaga Bodi iliyomaliza muda wake mjini Dodoma Mheshimiwa, Mhandisi Kamwelwe amesema mafanikio inayoyapata TANROADS yanatokana na ushirikiano uliojengwa kwa muda mrefu kati ya Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi.
“Hakikisheni mnatumia vizuri weledi na uzoefu wenu kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kwa sasa ili barabara zinazojengwa nchini ziwe bora na za viwango”, amesema Mhandisi Kamwelwe.
Ameitaka Bodi inayomaliza muda wake kutoa ushirikiano kwa Bodi mpya ili kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi na kufikia malengo ya kuiwezesha TANROADS kuwa Wakala bora wa barabara Barani Afrika.
Naye Katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhandisi Joseph Nyamhanga ameitaka Bodi mpya  kuhakikisha wafanyakazi wa TANROADS wanajengewa mazingira ya hamasa katika kufanyakazi zao ili kuongeza ubunifu.
“Hakikisheni mnaepuka rushwa na kuimarisha mifumo ya utendaji ili hadhi ya TANROADS iendelee kudumu”. Amesisitiza mhandisi Nyamhanga.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale ameishukuru Bodi inayomaliza muda wake kwa kazi nzuri na kuihakikishia ushirikiano Bodi mpya.
Bodi ya tatu ya TANROADS iliyozinduliwa leo inaundwa na Mwenyekiti Dakta, Damas Lucas Nyahoro na wajumbe saba ambao ni Johansen Kahatano, Devotha Mdachi, Eliud Nyauhenga, Fikiri Magafu, Eng. Happiness Mgalula, Mgonya Benedictor na Elinisaidie Msuli  na inatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment