VYAMA 14 VYAJITOKEZA KUGOMBEA UDIWANI, UBUNGE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 10 November 2018

VYAMA 14 VYAJITOKEZA KUGOMBEA UDIWANI, UBUNGE

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Giveness Aswile.

SUBIRA KASWAGA – AFISA HABARI NEC

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa jumla ya wagombea 13  walichukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge katika Majimbo ya Babati Mjini, Ukerewe, Simanjiro na Serengeti.

Akizungumza  ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu uteuzi huo Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Giveness Aswile amesema kuwa,  wagombea  hao wanatoka katika vyama sita vya siasa ambavyo ni AFP, CCM, CUF, NCCR Mageuzi, NRA na UDP.

Amesema kuwa, hadi muda wa mwisho wa uteuzi Novemba 02, mwaka huu saa 10:00 jioni, jumla ya wagombea wane wa Ubunge kutoka CCM, waliteuliwa na hivyo kutangazwa kuwa wamepita bila kupingwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

Wagombea hao walitangazwa kupita bila kupinga baada ya wanachama wengine kutoka vyama vilivyochukua fomu za uteuzi, kukosa sifa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kushindwa kurudisha fomu hizo kwa wakati na wengine kutojaza fomu hizo kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutojaza fomu ya kuheshimu na kuyazingatia maaadili ya uchaguzi

Aidha kwa upande wa udiwani katika kata 47 za Tanzania Bara, Aswile ameeleza kuwa, vyama 14 vya siasa vilishiriki ambapo wanachama 102 kutoka vyama hicvyo walichukua fomu za uteuzi.

“Vyama vilivyoshiriki ni AAFP, ACT – WAZALENDO, ADC, CCK, CCM, CHADEMA, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, NCCR – Mageuzi, NRA, SAU, TLP, UDP na UPDP” alisema Aswile na kufafanua kuwa,

Hadi Novemba 03, 2018 saa 10:00 jioni wanachama 73 tu ndio waliorejesha fomu na kuteuliwa kuwa wagombea Udiwani.

Wanachama wengine 29 hawakuteuliwa kuwa wagombea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kurejesha fomu za uteuzi, kutojaza fomu za uteuzi kwa usahihi, kutosaini fomu za kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi na kukosa sifa za kugombea udiwani kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Aswile amefafanua kuwa wagombea 15 wa nafasi ya Udiwani waliwekewa pingamizi kwa Msimamizi wa Uchaguzi na kupelekea wagombea 9 kuenguliwa kutoka katika orodha ya wagombea wa nafasi ya udiwani.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea rufaa mbili kutoka kwa Wagombea Udiwani wa Kata ya Muhinda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Kata ya Mnyamani iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wakipinga maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi kuwaondoa katika kugombea udiwani.

Aidha, katika kikao cha Tume kilichofanyika Novemba 09, 2018 kimeridhia rufaa moja ya mgombea Udiwani wa CUF katika kata ya Muhinda Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na hivyo kumrudisha mgombea katika nafasi hiyo.

“Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi katika kata ya Mnyamani Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ya kumuondoa mgombea wa CUF katika orodha ya wagombea na hivyo mgombea kuendelea kuenguliwa kugombea udiwani” alisema Aswile.

Aidha, katika kata 47 jumla ya wagombea udiwani katika kata 41 wamepita bila kupingwa na hivyo ni kata sita tu ndizo zitakazofanya uchaguzi Mdogo  tarehe 02, Desemba mwaka huu.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Nkoanekoli iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Kivinje/Singino, Mteja, Somanga, Mitole zote katika Halmashauri ya Kilwa na kata ya Butimba iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Kampeni za uchaguzi zimeanza tarehe 04 Novemba 2018 na zitakamilika tarehe 01 Desemba siku moja kabla ya uchaguzi.

Aswile amevikumbusha vyama vya siasa na wagombea kuheshimu Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 wakati wote wa kampeni na hata siku ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment