WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wahakikishe wanasimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao bila ya woga.
Kadhalika, Waziri Mkuu amemtaka kila mtumishi wa umma nchini awajibike katika kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.
Waziri Mkuu aliyasema hayo Novemba 27, 2018 alipozungumza na watumishi, viongozi wa mkoa, wilaya ya Geita na taasisi za umma katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mji Geita.
“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”
Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza watumishi wa umma hususani Wakuu wa Idara wahakikishe wanakuwa na kitabu cha Ilani ya Uchanguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wapate muelekeo wa utekelezaji washughuli zao.
Waziri Mkuu amesema kitabu cha Ilani ya uchanguzi cha CCM 2015/2020 kina maelekezo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo kila idara inatakiwa kuangalia maelekezo yaliyotolewa kuhusu idara husika na kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake watayafanyia kazi maelekezo yote ambayo ameyatoa.
No comments:
Post a Comment