SERIKALI KUWANUFAISHA WACHIMBAJI WADOGO-MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 29 November 2018

SERIKALI KUWANUFAISHA WACHIMBAJI WADOGO-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Ilembela wilayani Mbogwe akiwa katika ziara ya mkoa wa Geita, Novemba 29, 2018. (Picha na Ofisi  ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa Hadhara kwenye Kiwanja cha Shule ya Msingi ya Masumbwe wilayani Mbogwe, Novemba 29, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia Mkutano wa Hadhara kwenye Kiwanja cha Shule ya Msingi ya Masumbwe wilayani Mbogwe, Novemba 29, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati mizuri kuhakikisha wananchi hususani wachimbaji wadogo wadogo wananufaika na uwepo wa rasilimali hiyo.

Hivyo, Waziri Mkuu amewashauri wachimbaji wadogo wadogo wajiunge katika vikundi ili Serikali iweze kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo mkopo ili waongeze mitaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Novemba 29, 2018 alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi jengo la halmashauri ya Mbogwe.

Amewahamasisha wachimbaji hao watumie taasisi mbalimbali za kifedha na kukopa fedha na kununua mitambo ya uchimbaji na uchenjuaji kwa lengo la kujiongozea tija.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Geita kwa ziara ya kikazi, amesema wachimbaji wadogo wadogo waendelee kuwa na imani na Serikali yao, kwa kuwa imewapangia mambo mazuri.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali imedhamilia kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Amesema katika kumaliza tatizo la maji Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni moja kwa ajili ya  uchimbaji visima virefu 11 na visima vifupi 43 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati ya kumaliza tatizo la maji nchini kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.

Waziri Mkuu amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi katika maeneo yote wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote nchini wakiwemo na wa wilaya ya Mbogwe wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.”

Kuhusua suala la wanafunzi kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito wilayani Mbogwe, Waziri Mkuu ameitaka jamii kukemea vitendo hivyo. Wanafunzi 54 wamepata ujauzito.

Amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu wanafunzi 20 wa shule za msingi na 34 wa sekondari wameacha shule baada ya kupata ujauzito.

“Hali ni mbaya, Mbogwe inatia aibu kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliopewa ujauzito. Naagiza msiwaguse wanafunzi wa kike ni moto utawaunguza. Tukikukamata jela miaka 30.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema wilaya ya Mbogwe inafanya vizuri katika sekta ya madini, ambapo ina viwanda 27 vya kuchenjulia dhahabu.

Amesema katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wadogo wanawezeshwa kufanya shughuli zao vizuri, Serikali imetenga eneo la hekta 547.64 kwa ajili ya kuwagawia wachimbaji hao.

Akizungumzia kuhusu leseni za uchimbaji mkoani Geita amesema kuna jumla ya leseni 971 za uchimbaji mdogo wa madini na kati yake zinazofanyakazi ni leseni 184 tu.

Waziri huyo amewataka wachimbaji wadogo wadogo waendelee na shughuli zao za uchimbaji kwenye maeneo yao waliyopangiwa na kwamba hakuna atakayewaondoa.

Awali, Waziri Mkuu alikagua na kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mbogwe katika kijiji cha Kasosobe. Ujenzi huo utagharimu sh. bilioni 4.3. Pia alikagua mradi wa uboreshaji miundombinu na kuzindua maabara ya Kituo cha Afya Masumbwe.

No comments:

Post a Comment