UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA WAUWA 17 MKOANI RUKWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 4 October 2018

UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA WAUWA 17 MKOANI RUKWA

Mbwa wakipata chanjo.

WATU 17 wamefariki Mkoani Rukwa katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaosababishwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la “Lyssavirus” ambapo hushambulia mfumo wa fahamu na kusababisha kifo kwa binadamu na mnyama.
Hayo yamejulikana katika maadhimisho ya siku ya kuhamasisha udhibiti wa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa duniani yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya Nelson Mandela Manispaa ya Sumbawanga mwishoni mwa mwezi wa tisa, mwaka 2018.
Akisoma taarifa fupi ya ugonjwa huo mtaalamu wa magonjwa ya wanyama wa Mkoa Dkt. Respich Maengo amefafanua kuwa ugonjwa huo pia husambazwa na paka ambapo mtu aking’atwa au kukwaruzwa na paka mwenye kichaa pia husababisha binadamu kuupata ugonjwa huo.
“Mbwa waliopata chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa Mkoani Rukwa ni asilimia 14.6 ambao ni mbwa wachache sana na kati ya paka 9,514 waliopo, hakuna hata paka mmoja aliyepata chanjo hiyo, hii inaonyesha wazi kuwa wananchi hawaijali mifugo yao,” Alisema.
Maengo alieleza dalili za ugonjwa huo kwa binadamu kuwa mwanzoni hazieleweki vizuri kwani huanza kwa maumivu ya kichwa, homa na kuchoka kwa mwili na hatimae unavyoendelea mgonjwa huanza kukosa usingizi, kuwa na hasira na kuchanganyikiwa, kutokwa na mate mengi, kushindwa kumeza chakula, kuogopa kuangalia maji na kasha kufariki.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kuchanja si chini ya ailimia 70 ya mbwa wote, na katika Mkoa wa Rukwa mbwa waliochanjwa mwaka 2017/2018 ni 6,017 sawa na asilimia 14.6, huku Manispaa ya Sumbawanga ikiwa imechanja 30.5%, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga 15.3%, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo 6.3%, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi 7.3%.
Mwaka 2017/2018 watu walioumwa na mbwa ni 1,050 na vifo ni 17. Maadhimisho ya mwaka huu yanaendeshwa na kauli mbiu “Ugonjwa wa kichaa cha mbwa: Sambaza ujumbe okoa Maisha.”

No comments:

Post a Comment