Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akipata maelezo
kuhusu Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kwa Mhandisi wa Usafirishaji
Masafa wa TTCL, Marwa Chacha wakati wa ziara yake ya kukagua namna Mkongo huo
unavyopeleka mawasiliano Burundi kwenye kituo cha Biharamulo, Kagera.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akipata
maelezo kutoka kwa Afisa Mfawidhi wa Forodha wa Kituo cha Huduma cha Pamoja,
Mtukula Bwana Mohammed Shamte (wa pili kulia) kuhusu namna Mkongo wa taifa wa
Mawasiliano unavyowawezesha kusafirisha taarifa na data za wateja na bidhaa
baina ya Tanzania na Uganda wakati wa ziara yake Mtukula, Kagera.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano (wa pili kushoto) Mhandisi Atashasta Nditiye akikagua
tundu la Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
kituo cha Rusumo linalopeleka mawasiliano kutoka Tanzania kwenda Rwanda.
Mwenye koti nyeusi ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Wizarani, Mulembwa Munaku na wa nne
kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali, Michael Mntenjele.
|
MKONGO wa Taifa wa Mawasiliano umeongeza makusanyo ya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maeneo ya mipakani mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi na DRC Congo.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara
yake ya kukagua Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye kituo cha mpakani cha
Mtukula ambacho kinawezesha usafirishaji wa taarifa na data za wateja na bidhaa
kutoka Tanzania kwenda nchi jirani ya Uganda.
Nditiye amesema kuwa,
“maeneo ya mipakani ndi lango la kuongeza mapato na kukuza uchumi wan chi yetu,
niwatake muendelee na kasi hii ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kutumia
Kituo cha Pamoja cha Huduma ambapo tayari kwa kipindi cha miezi mitatu ya
mwanzo wa mwaka wa fedha wa 2018/2019, mwezi Julai hadi Septemba, 2018 mapato
yameongezeka zaidi ya asilimia 100 kwa mwezi na kufikia asilimia 150”.
Naye Afisa Mfawidhi wa
Forodha wa Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Mtukula, Bwana Mohammed Shamte
amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, malengo yao ni kukusanya kiasi
cha shilingi bilioni 15.9 kwa mwaka ambapo tayari imeonekana kiwango hicho
kitafikiwa kwa kuwa tayari kwa mwezi wanakusanya shilingi bilioni 1.3 ambazo ni
wastani wa asilimia 110 hadi 150 ya makusanyo kwa mwezi ambayo yanavuka
malengo.
“Baada ya Serikali
kuweka Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, umeongeza spidi na uhakika wa
kusafirisha taarifa na data tofauti na hapo awali tulipokuwa tunatumia
satelaiti, hivyo Mkongo umewezesha ongezeko la mapato,” amesema Shamte.
Nditiye ameongeza kuwa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umebadilisha sekta ya mawasiliano nchini na
kwenye nchi za jirani zilizounganishwa na Mkongo huo za Uganda, Rwanda,
Burundi, Kenya na DRC Congo ambapo wanafurahia huduma za mawasiliano. “Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano lazima ulindwe, ni kama reli au barabara, na
mawasiliano ni uchumi na maendeleo ambapo unaingiza mapato kwa Serikali yetu,”
amesema Nditiye.
Pia, amewataka wafanyakazi
wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) waendelee kuutunza na
kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuwa ni watu sahihi, wana utaalamu
na ujuzi wa kutosha kufanya kazi na Serikali imewaamini na kuwapa jukumu hilo
kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni usalama hivyo ukicheza na mawasiliano nchi
inasambaratika.
Wakiwasilisha
changamoto za mawasiliano kwa Nditiye, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Misenyi Bi. Thabitha Solomoni amesema kuwa wakati mwingine mtandao
unakwenda taratibu au kukosekana hivyo kuathiri usafirishaji wa taarifa na data
za watumishi kwa Serikali wa malipo na masuala ya watumishi.
Naye Meneja wa TTCL
Mkoa wa Kagera Bi. Irene Shayo amejibu changamoto hio kwa kusema kuwa
inategemea aina ya kifurushi ambacho Halmashauri husika imenunua na
wanachotumia. Ametoa rai kwa Halamshauri kutumia wataalamu wao kufahamu uwezo
wa mtandao wa intaneti wanaotumia ili uweze kuendana na mahitaji na ukubwa wa
taarifa au data wanazotuma au kupokea, hivyo Ofisi za Serikali zizingatie ubora
wa huduma kuendana na mahitaji yao na TTCL ina ofisi zake nchi nzima, wako
tayari kuwahudumia.
Nditiye amepokea
changamoto hiyo kuhusu spidi ya intaneti kwenye ofisi zao na amewataka
wataalamu wa TEHAMA kupeleka mahitaji
sahihi ya mtandao wa intaneti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zao na TTCL wako
tayari kushauri ili mahitaji yanayotakiwa yaweze kutolewa na TTCL kuendana na
mahitaji stahiki.
Naye Mkurugenzi wa
TEHAMA, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bwana Mulembwa Munaku
amewataka maafisa TEHAMA wote kufungia mitandao ya kijamii muda wa saa za kazi
ili mtandao wa intaneti uweze kutumika vizuri kwa matumiz ya Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemweleza Nditiye kuwa bado hakuna
mawasiliano ya kuridhisha kwenye maeneo mbali mbali ya mkoa huo licha ya kwamba
makampuni yote ya mawasiliano yapo ila bado kuna changamoto ya upatikanaji wa
mawasiliano ya uhakika kwenye mkoa huo.
Akitoa ufafanuzi
kuhusu changamoto hiyo, Nditiye amesema kuwa tayari Serikali imechukua hatua
kuhusu jambo hilo kwa kuongeza minara ya mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani
ambapo mawasiliano ni hafifu kwa kuwaelekeza wataalamu wa Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote kufika kwenye maeneo hayo, kufanya tathmini na kupeleka mawasiliano
kwa kuwa hadi sasa watanzania wanapata mawasiliano kwa kiwango cha asilimia 94
isipokuwa maeneo machache.
Pia ameipa TTCL mwezi
mmoja kuhakikisha vocha na laini za TTCL zinapatikana nchi nzima ili
kuwawezesha watanzania kuwasiliana kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni usalama.
Nditiye amefanya ziara
hiyo ya kukagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye vituo vya
mpakani vya Kabanga, Rusumo Mtukula na Biharamulo.
No comments:
Post a Comment