LISHE DUNI NA ULAJI USIOFAA NI ADUI WA MAENDELEO NCHINI - MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 21 September 2018

LISHE DUNI NA ULAJI USIOFAA NI ADUI WA MAENDELEO NCHINI - MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihutubia wananchi wa Kondoa Mji, kwenye Mkutano wa hadhara, akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Dodoma, Septemba 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

*Asema ni chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza saratani, kisukari na moyo 

MAGONJWA yasiyoambukiza yanachangia  kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya maendeleo yetu kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno, si kwa kaya zinazoathirika tu bali kwa Taifa zima. 

Lishe duni pamoja na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususan kwa vijana na watu wazima; ambao ndiyo nguvu kazi kwa Taifa letu.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati akifungua mkutano wa tano wa wadau wa masuala ya lishe,  jijini Dodoma. Alisema ni muhimu wadau hao kuweka mikakati kupunguza kasi ya ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

Waziri Mkuu alisema magonjwa hayo yanapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha. Ni jambo lisilopingika kuwa hatua za kukabiliana na magonjwa ya kusendeka (mfano matatizo ya moyo, saratani, kisukari na shinikizo kubwa la damu), zinapaswa kuchukuliwa.

Alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ni kujenga uchumi wa viwanda ambao utatuwezesha kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ni muhimu suala la lishe bora likapewa kipaumbele. 

Alisema kauli mbiu ya mkutano huo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Lishe Bora ni Msingi wa Kuendeleza Nguvu Kazi yenye Tija” inatoa hisia chanya ya kufikia azma hiyo kwa kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea sana uwepo wa nguvu kazi ya kutosha na madhubuti. 

Alifafanua kuwa miongoni mwa matatizo ya lishe duni ni pamoja na upungufu mkubwa wa vitamini na madini kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano (5), wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito, vijana balehe pamoja na wakina baba.

Waziri Mkuu alisema kuwa ni dhahiri kuwa tunahitaji kuanzisha viwanda vitakavyozalisha vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu ili kurahisisha upatikanaji wa vyakula hivyo katika jamii zetu. 

“Nitoe wito kwa wadau wote hususan sekta binafsi kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika viwanda vya usindikaji wa vyakula vinavyozingatia viwango vya ubora. Niwahakikishie kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji, kwa hiyo, tumieni kikamilifu nafasi hiyo.”

Alisema kwa pamoja, wanaweza kuimarisha mikakati yao ya kuivusha nchi na watu wake kutoka katika lindi la umaskini na kujenga nguvu kazi imara itakayoweza kuhimili changamoto za maendeleo ya viwanda. 

Waziri Mkuu anatumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wote, waendelee kuiunga mkono Serikali kwa kuwekeza katika utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ambayo inalenga kuboresha hali ya chakula na lishe miongoni mwa jamii, hususan kwa watoto, wanawake walio katika umri wa kuzaa, vijana balehe na watu wenye mahitaji maalum kilishe.

“Kwa msingi huo, Serikali imejumuisha masuala ya lishe katika Mpango wake Jumuishi wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021), kama eneo la kipaumbele katika kuboresha na kuendeleza nguvu kazi ya Taifa.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa “dhamira ya Serikali ni kutokomeza aina zote za utapiamlo kwa kuwekeza na kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote kushiriki katika kuchangia utekelezaji wa afua za lishe nchini ambazo zina matokeo ya haraka miongoni mwa makundi yote yanayoathirika.”

Alisema jitihada hizo zinalenga kutimiza azma ya Baraza la Umoja wa Mataifa la “Muongo wa Kuchukua Hatua katika Masuala ya Lishe - Decade of Action on Nutrition” ya mwaka 2016 hadi 2025 na pia kuwezesha kufikiwa kwa Malengo yote 17 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu (United Nations Sustainable Development Goals).  

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutilia mkazo suala la uhamasishaji miongoni mwa watunga sera na viongozi katika ngazi mbalimbali kuhusu masuala yote yanayohusiana na lishe kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala hayo. 

Alisema juhudi hizo zinaenda sambamba na utoaji wa elimu sahihi ya lishe kwa umma kwani tunaamini kuwa Watanzania wakielimishwa vizuri kuhusu masuala haya itachangia kuleta mabadiliko chanya katika jamii pamoja na taasisi zetu kwa ujumla. 

Alisema Serikali imeendelea kuongeza rasilimali kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza masuala ya lishe hususan katika ngazi za mikoa na halmashauri, ambapo takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko kutoka wastani wa sh. milioni 65 mwaka 2011/2012 hadi kufikia sh. milioni 219 mwaka 2016/2017. 

Kwa mwaka 2017/2018 Serikali ilikadiria kutumia jumla ya sh. billioni 11 katika utekelezaji wa masuala ya lishe katika ngazi ya halmashauri, hivyo hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2017/2018, kiasi cha sh. bilioni mbili zilitolewa na kutumika. 

Kadhalika, Waziri Mkuu aliendelea kuhimiza kuhusu suala la kutenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa idadi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika Halmashauri zetu kupitia mapato ya ndani ili ziweze kutumika katika kutekeleza Afua hizo kwenye Halmashauri husika. 

Aliwahakikishia wadau hao kuwa, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Afua za Lishe kama zilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe 2016/2017 - 2020/2021; kwa kadiri hali itakavyoruhusu.

“Nitoe rai kwa Watendaji Wakuu wote katika Wizara husika, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, asasi za kijamii; kila mmoja kwa nafasi yake au mamlaka yake, kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe.” 

Alisema mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa afua zilizoainishwa katika mpango huo zinajumuishwa katika mipango na bajeti zao za kila mwaka, sambamba na kutoa fedha zilizopangwa kwa ajili ya utekelezaji. 

Waziri Mkuu alisisitiza tena kuwa kila mdau anayeshiriki katika utekelezaji wa shughuli za lishe nchini aoneshe bayana mchango wake katika kukabiliana na utapiamlo nchini ili Taifa liweze kufikia malengo tuliyojiwekea. 

Alisema ili wahakikishe hatua tunazochokua katika mapambano dhidi ya utapiamlo zinaleta matokeo kama walivyopanga na zinawanufaisha au zinawafikia walengwa, aliwaagiza  viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali kutambua wajibu wao na kushiriki kikamilifu katika kudhibiti na kukabiliana na athari za utapiamlo katika maeneo yao. 

Pia, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wa Serikali katika ngazi za mbalimbali wafanye tathmini ya ufanisi wa hatua wanazochukua na watoe taarifa za ufanisi au changamoto mara kwa mara. 

Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama  alisema ushirikishwaji wa wadau kwenye masuala ya lishe umeongezeka na wanashuhudia wadau wengi wa maendeleo wakionesha nia na wengine kuwekeza katika masuala ya lishe nchini.

 Aidha, Waziri Jenista alisema wameweza kuratibu wa uanzishwaji wa mabaraza mbalimbali yanayojadili masuala ya lishe likiwemo baraza la sekta binafsi ambao wana mchango mkubwa katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kutokomeza utapiamlo inafikiwa. 

Alisema hatua hizo kwa kiasi kikubwa zimechangia kupunguza viwango vya utapiamlo pamoja na idadi ya vifo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. “Mfano mzuri ni pale tulipopunguza udumavu kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.4 mwaka 2016.” 

Alisema Taifa linahitaji nguvu kazi imara itakayohimili ushindani katika soko la ajira na kuendeleza Tanzania ya Viwanda. Nguvu kazi hiyo inaanza kujengwa kwa kuimarisha lishe bora hususan kuanzia pale mama anapokuwa mjamzito hadi mtoto anapofika miaka miwili. 

Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema viwango vya matatizo ya lishe vimepungua kwa baadhi ya viashiria ingawa si kwa kiasi cha kuridhisha.

Alitaja moja ya viashiria vya kupungua kwa matatizo ya lishe ni kushuka kwa tatizo la udumavu, ambapo kwa sasa kuna wastani wa watoto watatu wenye udumavu kati ya watoto 10 walio katika umri chini ya miaka mitano.

Waziri Ummy alisema kuwa udumavu huathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na kupunguza ufanisi wake katika maisha yake ya utu uzima.

Alitaja mikoa ambayo imeathiriwa zaidi na tatizo hilo la lishe ni pamoja na Rukwa, Njombe, Ruvuma, Iringa, Kagera, Mwanza na Geita, ambayo ina wastani wa zaidi ya asilimia 40. Mikoa hiyo ni kati ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa chakula nchini.

“Ni dhahiri kuwa, utatuzi wa suala hili unahitaji mbinu na hatua za haraka pamoja na ushirikiano wa kila mmoja wetu. Kulingana na takwimu za kidemografia na afya ya mwaka 2015/2016, watoto 106,000 wana utapiamlo mkali ukilinganisha na watoto 340,000 wenye utapiamlo wa kadiri.”

Alisema idadi hiyo inaashiria kuwa watoto hao wenye utapiamlo mkali wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha, ambapo hadi sasa changamoto kubwa waliyonayo ipo katika utambuzi wa tatizo, utoaji wa rufaa, upatikanaji wa chakula dawa na utoaji wa matibabu sahihi kwa watoto wenye tatizo hilo.

Kadhalika, Waziri Ummy alisema bado kuna hospitali chache zenye uwezo wa kutoa huduma ya matibabu ya utapiamlo mkali. Juhudi zinaendelea kuhakikisha hospitali zote nchini zinajengewa uwezo wa kutoa huduma hizo muhimu ili kuokoa maisha ya watoto walioathirika na utapiamlo mkali.

No comments:

Post a Comment