WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amezindua rasmi kazi ya utandikaji wa reli ya kisasa ya SGR kwenye eneo la Soga lililopo mkoani Pwani ambapo reli hiyo inajengwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa umbali wa kilomita 300 na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa.
Kamwelwe amesema kuwa reli hiyo yenye jumla ya kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni kwa ajili ya njia ya reli ambayo itakuwa na umbali wa kilomita 205 na kilomita 95 ni kwa ajili ya reli kupishana ambapo reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo kiasi cha tani milioni 17,000 kwa mwaka ambapo nchi yetu imeingia mkataba wa kujenga reli hiyo na kampuni ya Yapi Merkezi ya kutoka nchini Uturuki na kusimamiwa na mshauri mwelekezi wa kutoka nchini Japan kwa kushirikiana na kampuni ya kizalendo ya hapa nchini kwetu. Reli hiyo itaendeshwa kwa kutumia umeme na itakuwa na spidi ya kilomita 160 kwa saa.
Ameongeza kuwa Serikali inazalisha mataruma kwenye kiwanda chake yenyewe kilichopo Soga mkoa wa Pwani na vifaa vingine vya ujenzi wa reli hiyo kama vile sementi, mchanga na kokoto vyote vinapatikana hapa nchini. Amefafanua kuwa Serikali iliagiza reli peke yake kutoka nchini Japan ambapo kiasi cha tani 7,250 ziliingizwa nchini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita ambapo reli hizo zitatumika kujenga reli hiyo ya kisasa ya SGR kwa ukubwa wa kilomita 60.
Amesema kuwa itafika siku ambapo nchi itachimba chuma kutoka kwenye mgodi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa ya SGR badala ya kuendelea kuagiza reli kutoka nje ya nchi.
Kamwelwe amewataka wananchi watambue jitihada za Mhe. Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhimiza wananchi walipe kodi ili Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iweze kukusanya kodi na mapato ambayo yanatuwezesha kama nchi kutumia fedha zetu wenyewe kujenga reli hiyo na tumewajiri wataalam wa kujenga reli hiyo na mkataba umesainiwa mwaka jana kwa ajili ya kujenga kilomita 300 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. “tumewaajiri hawa Yapi Merkezi na kazi hii wanatufanyia sisi wenyewe,” amesisitiza Kamwelwe.
Katika hatua nyingine, Kamwelwe ametoa wito kwa watanzania waliopata nafasi ya kufanya kazi kwenye ujenzi wa reli hiyo watumie utaalamu wao vizuri ili nchi iweze kufanya kazi zake yenyewe na uzalendo uzingatiwe ili tuweze kufikia hatua ya kutumia wakandarasi wetu wa ndani kufanya kila kitu na utaratibu utaangaliwa ili wakandarasi wetu wafanye kazi hizi wao wenyewe kwa kuwa kila kitu kinapatikana hapa nchini.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro Mhandisi Maizo Mgedzi amesema kuwa mradi huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu ya usanifu, kuchukua ardhi baada ya kufanya tathmini na kulipa fidia na kujenga reli yenyewe ikiwa ni pamoja na kuandaa mfumo wa uendeshaji na matengenezo ya reli hiyo ambapo mitambo na watalaam wa kuendesha reli hiyo vitahitajika.
Hadi hivi sasa vijana 60 wazalendo wenye utaalamu na ujuzi wa uhandisi wamepata mafunzo nchini na watapelekwa nje ya nchi kwenye reli na viwanda vinavyofanya kazi ili waweze kuongeza ujuzi na maarifa ya kuendesha reli hii na Shirika litaendelea kuandaa vijana wengine 160 kwa ajili ya uendeshaji wa reli hiyo.
Ameongeza kuwa reli hiyo itatumia umeme na sio dizeli ambapo TANESCO imepewa jukumu la kutoa umeme kutoka kwenye gridi ya taifa na kuleta kwenye mfumo wa reli ya kisasa ya SGR ambapo jumla ya megawati 160 zitahitajika kuendesha reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Shirika la Reli Tanzania litakuwa na jukumu la uhandisi ujenzi, madaraja, mifumo na njia kwa ajili ya kuendesha reli ya kisasa ya SGR.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment