SERIKALI imesema inatarajia
kutangaza katika Gazeti la Serikali msitu wa Mwalimu Nyerere uliopo Butiama mkoani
Mara kuwa eneo lindwa kimazingira, kufuatia ahadi iliyotolewa mwaka jana wakati
wa kilele cha Siku ya Mazingira Duniani
iliyofanyika Butiama mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba mara
baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na
mwakilishi wa familia hiyo Bw. Madaraka Nyerere.
Bw. Nyerere amesema kuwa
kama familia watafurahi sana kwa eneo hilo kutangazwa kama eneo lindwa ikiwa ni
pamoja na kuweka taratibu za matumizi sahihi ya uvunaji wa rasilimali ndani ya
msitu huo na kutoa zuio kwa baadhi ya shughuli za kibinadamu isipokuwa kwa
kibali maalumu tu.
Akiwa katika mwendelezo wa
ziara ya kukagua masuala ya usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya mazingira
nchini, Waziri Makamba amesema kuwa lengo la kuhifadhi baadhi ya maeneo nchini
ni kuhakikisha kuwa yanakuwa na usimamizi endelevu kwa manufaa ya wote.
Awali akiwa katika Manispaa
ya Musoma Mkoani Mara Waziri Makamba ametembelea Mlima Mukendo uliopo Mtaa wa
Nyerere, Kata ya Mukendo na kuridhia ombi wa Baraza la Madiwani la kuomba msitu
huo uhifadhiwe kwa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
“Nawapongeza sana Uongozi wa
Mkoa wa Mara, wao wameenda mbali zaidi kwa kupitisha azimio hili katika Baraza
la Madiwani, hii inatupa sisi msukumo wa kufanya jambo hili kwa haraka zaidi,
sisi kama Serikali tutaleta rasimu ya tangazo la gazeti mapema iwezekanavyo ili
tukubaliane masharti na vigezo tutakavyoweka kabla ya kulitangaza rasmi katika
gazeti la Serikali” Makamba alisisitiza.
Katika hatua nyingine,
Waziri Makamba ametoa rai kwa ungozi wa Mkoa wa Mara haraka iwezekanavyo
kupendekeza majina ya maafisa wanaofaa kuteuliwa kuwa wakaguzi wa mazingira na
kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC)
ndani ya mwezi mmoja kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa Mazingira walioteuliwa na
watakaoteuliwa ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Mratibu wa Mazingira
Kanda ya Ziwa, isipite tarehe 30/09/2018 kabla ya wakaguzi hawa kupatiwa
mafunzo na vitambulisho” Makamba alisisitiza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara
Mhe. Adam Malima amesema Mkoa wake unalenga kutekeleza kwa vitendo kampeni ya
kuifanya ‘Mara kuwa ya kijani’ na mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kupanda
miti milioni 10 ndani ya miaka miwili.
Katika kuunga mkono
jitihada kubwa za Mkoa wa Mara katika kampeni
ya kupanda miti Waziri Makamba ameahidi kutoa viriba Milioni Moja vyenye
thamani ya Shilingi Milioni 5 na laki 5. Waziri Makamba anaendelea na ziara
yake Mkoani Mara kwa kutembelea Wilaya ya Serengeti.
No comments:
Post a Comment