VIJANA PAROKIA MBURAHATI WAJA NA WAZO BUNIFU KUUNGANISHA BURUDANI NA UJENZI WA KANISA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 9 March 2026

VIJANA PAROKIA MBURAHATI WAJA NA WAZO BUNIFU KUUNGANISHA BURUDANI NA UJENZI WA KANISA

Na Frida Manga 

VIJANA wa Parokia ya Familia Takatifu Mburahati katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wamekuja na wazo bunifu la kuunganisha burudani na ujenzi wa Kanisa kupitia Tamasha maalum lijulikanalo kama “Burudika Kiujenzi.”

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika tarehe 10 Mei mwaka huu katika viwanja vya parokia hiyo, likiwa na lengo la kukusanya fedha za kuendeleza ujenzi wa Kanisa pamoja na kuhamasisha waamini, hususan vijana, kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Kanisa lao.

Uzinduzi wa tamasha hilo umefanyika parokiani hapo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Jumapili ya Tatu ya Kwaresma, ambapo Paroko wa parokia hiyo, Padri Ephraim Ogha, mmisionari wa Shirika la Wakamiliani, aliwahimiza waamini kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo ambalo mbali na burudani pia linakusudia kusaidia jitihada za ujenzi wa Kanisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, William Magambi, amesema matarajio yao ni kukusanya kiasi cha shilingi milioni 40, fedha zitakazotumika kuendeleza ujenzi wa Kanisa la parokia hiyo.

Naye Mratibu wa Tamasha hilo na mbeba maono, Mugabe Beka, amesema wazo la tamasha hilo lilizaliwa kutokana na hamu ya kuona vijana wanashiriki katika ujenzi wa Kanisa lao kwa njia inayowavutia, huku wakipata nafasi ya kuburudika.

“Nilitafakari namna ambavyo vijana wanaweza kushiriki katika ujenzi wa Kanisa huku wakiburudika, ndipo wazo la Burudika Kiujenzi likazaliwa,” amesema.

Tamasha hilo litafanyika katika viwanja vya parokia hiyo ambapo gharama za kushiriki ni Shilingi 15,000, 20,000 na 100,000 kulingana na aina ya tiketi.

No comments:

Post a Comment