MAFANIKIO YA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YANAHITAJI USHIRIKIANO - MASAUNI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 15 March 2026

MAFANIKIO YA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YANAHITAJI USHIRIKIANO - MASAUNI


Na Mwandishi Wetu, Geita

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema mafanikio ya ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, Serikali, Taasisi za elimu, Sekta binafsi, Asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla katika kufikia lengo la Tanzania yenye mazingira safi, afya bora na maendeleo endelevu.

Amesema Ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda kubwa duniani. Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 2.1 hadi 2.3 duniani bado wanaendelea kutumia kuni, mkaa na mafuta, na nishati nyingine zinazochafua mazingira.

Mhe. Masauni ameyasema hayo Mkoa wa Geita, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Machi 14, 2026 wakati akikagua mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Geita ambayo ni miongoni mwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku iliyoachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa chini ya asilimia 20 ya kaya nchini ndizo zinazotumia nishati safi ya kupikia kwa kiwango kikubwa, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza juhudi katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

“Kwa kutambua changamoto hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 2034) unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.”

“Ni fahari kubwa kwa taifa letu kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametambuliwa kimataifa kama Kinara wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika.”

“Kupitia uongozi wake, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ajenda hii barani Afrika na duniani, ikiwemo kushiriki katika mikutano ya kimataifa na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya nishati safi ya kupikia. Kwa juhudi hizi, Tanzania pia imekuwa moja ya nchi zinazoongoza katika kutekeleza sera na mikakati ya kuharakisha upatikanaji wa nishati safi barani Afrika.” Amesema Mhe. Masauni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba amesema wameitikia wito wa tayari serikali wilayani humo wamekubaliana kuhakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanasaidia taasisi zinazopatikana wilayani hapo zinatumia nishati safi ya kupikia.

“Tunazo taasisi nyingine za elimu ambazo nazo zinatumia nishati safi ya kupikia ikiwa pamoja na wataalamu wetu kutembelea magereza zetu ili kuona namna gani nazo zinahama katika nishati wanazotumia sasa,” amesema Mhe. Komba.

Aidha Mkuu wa Shule hiyo Bi. Mwamini George Kagoma ameeleza kuwa shule hiyo ilianza matumizi ya Nishati safi ya kupikia kuanzia mwaka 2025 ambapo matumizi ya nishati hiyo yameleta manufaa mbalimbali ikiwa pamoja na kupunguza gharama ya ununuzi wa Kuni na Mkaa, kuokoa muda, kulinda afya kwa kupunguza hewa chafu na chakula kuiva kwa wakati na mazingira ya jiko kuwa safi.

No comments:

Post a Comment