JAMHURI ya Muungano wa Tanzania inatarajia kunufaika na ufadhili wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15,096,716 kupitia Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (United Nations Environment Program - UNEP), kuwezesha miradi ya kusaidia kuhimili athari za mabadiliko ya Tabia Nchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia katika maeneo ya vijijini.Hayo yamejili kwenye Mkutano wa Saba wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (High level Segment of the 7th Session of the United Nations Environment Assembly – UNEA-7) unaoendelea jijini Nairobi, Kenya ambapo Tanzania inashiriki, ikiwa ni moja ya nchi wanachama wa umoja huo.
Maeneo yatakayonufaika na miradi hiyo ni pamoja na bonde la Mto Wami na Ruvu ambapo zitatekelezwa programu za urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na usimamizi endelevu wa mabonde hayo. Vilevile vijiji mbalimbali vya mikoa ya Morogoro, Dodoma, Pwani, Arusha, Simiyu na Mara vinatarajiwa kunufaika na miradi mbalimbali ya kutatua changamoto za mazingira.
Miradi na programu zitakazotekelezwa zinalenga kuboresha uwezo wa jamii kukabiliana na athari zinazoendelea kuongezeka kutokana na mabadiliko ya Tabia Nchi, ikiwemo mafuriko, ukame, kupungua kwa uzalishaji wa kilimo, uharibifu wa vyanzo vya maji na mmomonyoko wa ardhi, ili kuongeza ustawi wa jamii na shughuli za uchumi.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi (Mb) akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuhusu umuhimu wa mataifa kuwa na jitihada za pamoja ili kukukabiliana na athari za madiliko ya Tabia Nchi.
“Hakuna nchi inayoweza kujenga ustahimilivu peke yake. Ushirikiano, usawa wa kiteknolojia na ufadhili wa uhakika na unaotabirika ni masuala ya lazima. Kwa mataifa mengi yanayoendelea ikiwemo Tanzania, athari za kimazingira zinaendelea kuzidi uwezo wetu wa kukabiliana nazo. Hivyo, tunatoa wito kwa washirika wetu kuheshimu na kutimiza ahadi zao.” Ameeleza Mhe. Lukuvi.
Mkutano huo wa siku tano (Disemba 8 – 12, 2025) umefunguliwa rasmi na Rais wa Jumhuri ya Kenya Mheshimiwa Dkt. William Ruto, leo tarehe 11 Disemba 2025, ambapo pamoja na masuala mengine amesisitiza kuhusu, umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kulitazama zaidi Bara la Afrika katika ugawaji wa rasilimali zinazoelekezwa katika kukabiliana na athari za madiliko ya Tabia Nchi, kwa kuwa changamo za mazingira zinazidi uwezo wa uchumi na teknolojia ya Mataifa mengi barani.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Festo Dugange, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernard Kibesse na Maafisa Waandamizi wa Serikili, ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi.



No comments:
Post a Comment