Mkurugenzi wa Human Life International (HLI) Kanda ya Afrika' Kwa Nchi Zinazozungumza Kiingereza, EMIL HAGAMU.
Na Mwandishi Maalumu, Arusha
WAWAKILISHI wa shirika la kimataifa la kutetea uhai la Human Life International (HLI) Kanda ya Afrika Mashariki wanakutana mjini hapa kujadili Muswada wa Ujinsia na Afya ya Kizazi wa Mwaka 2024 wakisema haustahili kuingizwa wala kujadiliwa katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kwa kuwa hauna tija ya kimaendeleo kwa watu katika nchi za jumuiya hiyo.
Mkutano huo ulioanza juzi mjini hapa na kutarajiwa kuhitimishwa leo Jumapili unawashirikisha wawakilishi wa nchi nne za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.
Majadiliano na maazimio ya kuukataa muswada huo yatawasilishwa kwa Spika wa EALA.
Kama muswada huo utakataliwa usijadiliwe katika Bunge hilo itakuwa mara ya tatu kwani kwa mara ya kwanza ulikataliwa mwaka 2017 na kwa mara ya pili ulikataliwa mwaka 2021.
Wawakilishi na watetezi hao wa uhai wanategemea kutumia vyombo na taasisi mbalimbali kueleza wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kwa umoja wao na kupitia wabunge wa nchi zao waukatae.
Miongoni mwa mambo ambayo HLI Kanda ya Afrika Mashariki inatafakari na kuona hayana tija kwa nchi wanachama wa EAC ni pamoja na Kifungu cha 16 muswada huo kuhusu kutungwa kwa sheria kuruhusu utoaji mimba, elimu ya masuala ya ngono shuleni, kuhamasisha matumizi ya vidhibiti mimba, itikadi za ujinsia na haki ya vijana kupata huduma za uzazi wa mpango bila vikwazo.
Katika mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na wajumbe wanne ambao ni Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu; Makamu Mwenyekiti wa Prolife Tanzania, Elimina Kalunga; Mkufunzi na Msaidizi wa Prolife Tanzania, Castory Mdude na Mwakilishi wa Prolife Tanzania, Kanda ya Kaskazini, Agnes Ramadhani.
Wengine ni Mkurugenzi wa HLI nchini Uganda, Padri Jonathan Opio, Mkurugenzi wa HLI nchini Rwanda, Aloys Ndegeye na Mwakilishi wa HLI nchini Burundi, Revelien Ntezimana.
Katika michango yao wakati wa mjadala, watetezi hao wa uhai wamesema watu wa EAC wanayo masuala muhimu ya kushughulikiwa na bunge yakiwamo maendeleo ya miundombinu, afya bora, huduma za mawasiliano, elimu na umoja na si masuala yanayohusu ngono kwa vijana.
Hagamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa HLI Kanda ya Afrika kwa nchi zinazozungumza Kiingereza amesema: “Muswada unapingana na mila na desturi za watu wa Afrika Mashariki na ni kinyume cha malezi na mafundisho ya dini zetu za Uislamu na Ukristo.”
Akizungumza kwa njia ya mtandao, Ntezimana wa Burundi amesema muswada unaonesha kama vile shida na mahitaji ya watu wenye ulemevu ni kupanga uzazi kwa kutumia vidhibiti mimba ambavyo vinaweza kuwaongezea matatizo.
Amesema badala wawezeshwe na kusaidiwa kubuni njia za kujiwezesha kiuchumi na kupata huduma bora za kijamii kama elimu na afya bila vikwazo…”
Kwa upande wa Rwanda, Ndegeye amesema: “Muswada huu unadhamiria kuharibu kizazi cha baadaye cha watu wa EAC…”
Padri Opio kutoka Uganda amesema; “Muswada huu hauendani na nafasi na dhamira ya watu wa Afrika Mashariki.”

No comments:
Post a Comment