INEC YAWANOA WANAHABARI WAZALISHAJI MAUDHUI MITANDAONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 3 August 2025

INEC YAWANOA WANAHABARI WAZALISHAJI MAUDHUI MITANDAONI

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, akifungua warsha kwa wanahabari wazalishaji maudhui mtandaoni juu ya masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, iliyoandaliwa na INEC.


Baadhi ya washiriki wa warsha kwa wanahabari wazalishaji maudhui mtandaoni juu ya masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, iliyoandaliwa na INEC wakifuatilia mada anuai.

Sehemu ya washiriki wa warsha kwa wanahabari wazalishaji maudhui mtandaoni juu ya masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, iliyoandaliwa na INEC wakifuatilia mada anuai.


TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa mafunzo kwa wanahabari wazalishaji wa maudhui mitandaoni ili kuwaandaa kushiriki vema katika kutoa elimu kwa jamii na hasa kundi la vijana kushiriki kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa wale wenye sifa.

Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amewataka wazalishaji hao wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi huo.

Alisema INEC inatambua umuhimu wa wanahabari wanaozalisha maudhui mtandaoni na ndio maana umeamua kuwawezesha kwa mafunzo ili washiriki katika tukio la utoaji elimu na uhamasishaji wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya tukio la upigaji kura kuchagua viongozi wanaowataka.

“Tuna imani kuwa tutazidi kushirikiana nanyi kwa karibu zaidi, na mtatumia nafasi zenu kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa kupiga kura,” alisema Mhe. Jaji Mwambegele.

“Tume inathamini kazi yenu ya kuandaa, kuchapisha na kusambaza taarifa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali kama vile mitandao ya kijamii, blogu, tovuti na majukwaa ya video kama YouTube, ndio maana tumewaita kushirikiana nanyi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INEC, Bw. Kailima Ramadhani akiwasilisha mada yake kwa washiriki wa semina hiyo, aliwaomba kuhakikisha wanatumia mitandao hiyo kutoa habari sahihi, na zilizothibitishwa na kufanyiwa utafiti kwa wananchi ili kuepuka taharuki isiyo ya lazima kwa wasomaji.

Bw. Kailima amewataka wazalishaji hao wa maudhui mitandaoni kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikiwa ni pamoja na kuitumia kauli mbiu ya uchaguzi “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura” ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa ajili ya kupiga kura.

Alisema Tume itaendelea kutoa habari na elimu ya mpiga kura kupitia njia mbalimbali ikiwepo vikao na mikutano ya wadau wa uchaguzi, vyombo vya habari, kurasa za mitandao ya kijamii, magari ya matangazo na vipeperushi ili kuhakikisha elimu hiyo inasambaa na kumfikia kila mlengwa.

Aidha aliongeza kuwa jumla ya wapiga kura 37,655,559 wanatarajia kushirikia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku wapiga kura 36,650,932 wakitokea Tanzania Bara na wapiga kura 1,004,627 wakitokea Tanzania Zanzibar.

No comments:

Post a Comment