VETA YAWATUNUKU VYETI WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI 700 BAADA YA MAFUNZO MAALUM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 3 July 2025

VETA YAWATUNUKU VYETI WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI 700 BAADA YA MAFUNZO MAALUM

Mwezeshaji wa program hiyo, Debora Mwageni akizungumzia programu hiyo.

NA DUNSTAN MHILU

ZAIDI ya wafanyakazi wa majumbani 700 wamepatiwa mafunzo maalum na kutunukiwa vyeti na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi mahususi kwa kazi zao.

Hayo yameelezwa na Muwezeshaji wa mradi huo, Debora Mwageni alipozungumza na TheHabarii kuhusu mambo mbalmbali yanayotekelezwa na VETA katika kumuwezesha kijana kujikomboa kiuchumi.

Mafunzo hayo yanamwezesha mfanyakazi wa ndani kuwa na uwezo wa kushiriki majadiliano yenye lengo la kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kupata maslahi bora.

Debora amesema mradi huo ulianza Aprili mwaka jana na umepokelewa kwa muitikio mkubwa sana na wananchi na hivyo kuchangamkia fursa na hatimaye sasa wanatembea kifua mbele wakijua wanakitu cha kuwasaidia maishani.

“Wafanyakazi wa ndani wanasaidiwa kuelewa majukumu yao, haki na wajibu wao katika kazi wanazofanya hivyo kwa mafunzo haya yatakuwa yamewajengea uwezo zaidi na kujitabua wakiwa mahali pa kazi na hata baadaye katika maisha yakujitegemea” alisema Debora

Aidha, amesema kupitia mradi huo, wafanyakazi hao wanawezeshwa kupata ajira za kudumu, kulinda afya zao na kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama.

Mafunzo hayo yanahusisha masuala mbalimbali kama vile uandaaji wa chakula, usimamizi wa nyumba, usafi, kufua na kunyoosha nguo, pamoja na malezi ya watoto na wazee.

Debora aliongeza kuwa mafunzo pia yanawaandaa kwa ajili ya kufanya kazi katika nchi za nje kama vile Dubai, Oman, Denmark, Uingereza, Marekani na Italia.

“Tunawapa ujuzi wa stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi, pamoja na mbinu bora za kuwahudumia watu wanaoishi nao kwa ukarimu huku wakifahamu haki zao za msingi,” amesema.

Aliongeza kuwa wafanyakazi wa ndani ni sawa na wafanyakazi wengine, hivyo wanapaswa kupata heshima stahiki na kutambuliwa rasmi.

Debora aliwashauri Watanzania kujiwekea utamaduni wa kupata elimu na mafunzo kabla ya kuajiriwa ili kujiimarisha katika kazi zao.

“Kwakufanya hivyo kutasaidia kuepukana na kadhia ambazo zinazuilika kabla yakutokea madhara makubwa, hivyo basi wanaposikia mafunzo yoyote yale aidha yanahitaji fedha kidogo au hayahitaji fedha wasiache kushiriki,” amesema Debora.

No comments:

Post a Comment