Burudani ya ngoma za asili zikitolewa mbele ya Rais Samia.
KATIKA Uwanja wenye historia nene ya tamaduni, Uwanja wa Kisesa Jijini Mwanza, sauti za ngoma za jadi, mapembe ya asili na vishindo vya mizinga ya utamaduni vilisikika kwa mbwembwe huku hewa tulivu ikiwa imemzunguka kiongozi mkuu wa nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipohudhuria Tamasha la Utamaduni la Bulabo linalozidi kuwa kitovu cha heshima na ushawishi wa viongozi wa mila nchini.
Lakini si ngoma si ng'ombe waliokabidhiwa, wala si maigizo ya kikabila yaliyotikisa jukwaa – bali ni maneno yenye uzito wa kipekee yaliyotolewa na machifu hao yaligusa mioyo ya Watanzania na kuyatia alama ya historia ya taifa:
“Huyu ndiye damu yetu, huyu ndiye roho yetu – hataguswa!”
SAMIA ATOA WITO WA AMANI KWA WAGANGA NA VIONGOZI WA KIMILA
Akihutubia kwa sauti ya utulivu iliyojaa hekima na busara, Rais Samia hakusita kuwakumbusha viongozi wa kimila na waganga wa jadi juu ya jukumu lao nyeti katika kudumisha amani hasa kipindi hiki cha uchaguzi huku akiwaelekeza kwa sauti ya kirafiki lakini yenye msisitizo, alisema:
"Kipindi hiki wanaoomba nafasi mbalimbali za uongozi watawatembelea. Niwaombe sana msifanye ramli chonganishi kwa sababu hizo ndizo zinazovunja amani kwenye uchaguzi. Kama anakuja na fungu, we kula. Umemuona anashinda mwambie utashinda, umemuona hatashinda mwambie baba, we nenda tu mambo mazuri. We kula pesa yako, nenda kalale."
Kauli hiyo ilizua kicheko kizito lakini chenye tafakari miongoni mwa waliohudhuria tamasha hilo, huku ikionesha dhahiri namna Rais Samia anavyoujua utamaduni wa jamii ya kitanzania kwa undani na kutumia busara kuufikisha ujumbe wa kulinda amani bila kugusa imani au heshima ya mtu yeyote.
MACHIFU: “HATUTAKUACHA, HATUTAKUACHA!”
Ni katika jukwaa hilo la kihistoria ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu Antonia Tonisiza Sangalali, alitoa tamko la kihistoria lililosababisha kila mtu kusimama kwa heshima".
“Ni nani kama Samia? Tunaye rais muelewa, muadilifu, anatupenda, anaheshimu kila mtu, anamstiri kila mtu, anawaheshimu watu wote habagui. Rais huyu anatakiwa kufichwa roho yake ndani ya mioyo yetu. Tunakupenda Mama, tutakutetea, tutakulinda, na tutakuficha.” alisema Sangalali.
Sauti hiyo haikuhitimishwa tu kwa maneno matamu, bali ilifuatwa na kitendo cha machifu hao kumkabidhi Rais Samia ng’ombe watatu kama zawadi ya heshima, ishara ya mapenzi ya dhati kutoka kwa jamii ya viongozi wa kimila nchini.
“HUTAGUSWA!” – MACHIFU WATANGAZA ULINZI WA KIMILA
Wakizungumza kwa kauli moja, machifu waliahidi hakuna atakayemgusa Mama Samia na kwamba yeye ni kama moyo unaopeleka damu kwenye kila sehemu ya taifa. Kauli hiyo si tu iligusa mioyo ya waliohudhuria, bali ilitengeneza historia mpya ya uhusiano kati ya viongozi wa mila na dola:
“Ukiguswa tumeguswa, ukishikwa tumeshikwa. Hatuna silaha, lakini hakuna atakayekugusa. Hutaguswa! Tunasema katika hadhara hii ya Bujora, hakuna atakayekutikisa,” alisema mwenyekiti huyo.
Kauli hiyo ilikatisha pumzi za wengi waliokuwa wakifuatilia kwa makini tamasha hilo, huku ikitoa ujumbe mzito wa mshikamano wa kitaifa, upendo kwa kiongozi mkuu wa nchi na kuonyesha wazi kuwa tamaduni si tu mapambo ya historia, bali ni nguzo ya sasa na kesho ya taifa.
UTAMADUNI, AMANI NA MAENDELEO – VITU VITATU VYENYE ROHO MOJA
Tamasha la Bulabo limejipambanua kama jukwaa la kukuza utamaduni, lakini safari hii, limeenda mbali zaidi kwa kuibua mshikamano, mapenzi, maono na ujumbe wa amani kwa taifa. Ni tamasha lililounganisha ngoma za asili na midundo ya maendeleo, mizinga ya shangwe na sauti za hekima kutoka kwa viongozi wa mila.
Katika zama ambapo dunia inakumbwa na mitafaruku ya kisiasa na kikabila, Tanzania imeonesha njia mpya – njia ya kuwakumbatia wazee, viongozi wa kimila, na kuwasikiliza wale wanaoelewa sauti ya ardhi ya taifa hili tangu enzi za mababu.
HITIMISHO: MAMA SAMIA, “ROHO YA TAIFA”
Katika kila mdundo wa ngoma ya Kisukuma uliopigwa leo, katika kila neno lililotamkwa kwa heshima na imani, aliyejionesha kuwa mhimili wa taifa hili kwa sasa ni Mama Samia. Ameshikilia usukani kwa ustadi, ameiheshimu asili, amesikiliza wazee, na ameweka amani mbele ya kila jambo.
Kwa kauli za upendo na heshima walizozitoa Machifu, taifa limepata mzani wa maadili. Na kwa ujumbe wa Rais Samia kwa viongozi wa kimila, taifa limepata dira ya amani. Hakika, leo historia ya Tanzania imeandika ukurasa wa dhahabu katika
Uwanja wa Kisesa – ukurasa unaosomeka hivi:
“Hatuna silaha, lakini hakuna atakayekugusa. Mama Samia ni roho yetu – na roho haipigwi, haishikwi, haikatwi. Inaenziwa.”
Makala haya yameandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754-362990)


No comments:
Post a Comment